MBIO za hisani za kimataifa zilizoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) 'NBC Dodoma Marathon' zimefanikiwa kukusanya fedha zaidi ya shilingi Milioni 200 kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa akina mama huku ikishuhudiwa wanariadha kutoka Tanzania wakifanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo kwa kuibuka vinara kwenye mbio za Km 42 na Km 21.
Katika mbio hizo zilizofanyika jijini Dodoma hii leo na kupambwa na uwepo wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ilishuhudiwa mwanariadha Mtanzania Tumaini Habie akiiibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Km 42 upande wa wanaume baada ya kumaliza kwa muda wa saa 02:17:15, akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya Eyanae Paul aliyetumia muda wa saa 02:18:31. Mtanzania Abrahamu Too alimaliza katika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa saa 02:19:04.
Upande wa wanawake mshindi wa kwanza katika mbio za Km 42 ni Mkenya Cheruto Isgah aliyetumia muda wa saa 02:45:03 akifuatiwa na Watanzania Jackline Sakilu na Sara Ramadhani waliotumia muda wa saa 02:45:46 na 02:46:13 kila mmoja.
Mwariadha wa Kimataifa kutoka Tanzania Alphonce Simbu aliibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Km 21 baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:03:46, akifuatiwa na watanzania wengine katika nafasi ya pili na ya tatu ambao ni Joseph Panga pamoja na Daniel Giniki waliotumia muda wa saa 01:04:18 na 01:05:37 kila mmoja.
Upande wa wanawake mshindi wa kwanza katika mbio za km 21 ni Mtanzania Failuna Abdi aliyetumia muda wa saa 01:14:50 akifuatiwa na Wakenya Lelei Jepkemboi na Tanui Euliter waliotumia waliotumia muda wa saa 01:15:18 na 01:17:21
Katika mbio hizo ilishuhudiwa mshindi wa kwanza wa kilometa 42 kwa wanaume na wanawake kila mmoja akiondoka na Sh milioni 5.5 huku upande wa kilometa 21, mshindi akiondoka na kitita cha shilingi Milioni 3.5, wakati katika kilometa 10, mshindi alipewa Sh milioni 1.5 na mshindi wa kilometa tano alipewa Sh milioni 1.
Akikabidhi hundi ya mchango huo yenye thamani ya shilingi Milioni 200 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Julius Mwaiselage pamoja na zawadi kwa washindi wa mbio hizo, Waziri Bashungwa pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuandaa vema mbio hizo alisema licha ya faida nyingine za kimichezo umuhimu wa mbio hizo unapimwa zaidi katika lengo lake la kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi kwa kina mama.
“Tangu kuanzishwa kwa mbio hizi huu ukiwa ni msimu wa pili sasa, serikali imekuwa mstari wa mbele kuziunga mkono kutokana na dhima yake kuu ya kuwasaidia kina mama dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi. Tunashukuru kuona nia hiyo imefanikiwa na sasa tunakwenda kuokoa maisha ya maelfu ya kina mama kupitia jitihada za kimichezo.’’ Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw. Theobald Sabi aliwashukuru washiriki pamoja na wadhamini wa mbio hizo kwa kufanikisha lengo kuu la mbio hizo la kuchangia huduma za afya katika Hospitali ya Ocean Road, hasusani matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi, ambayo ndiyo inayoongoza kwa vifo vitokanavyo na saratani nchini.
Alisema kupitia mbio hizo mwaka jana waliweza kukusanya fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo na mwaka huu lengo lilikuwa ni kukusanya kiasi cha sh mil 200 zilizopatikana kupitia usajili wa washiriki wa mbio hizo pamoja na michango mbalimbali kutoka kwa wadhamini wa mbio hizo.
“Ndio maana pamoja na yote tunatumia fursa hii kujipongeza sisi sote tukiwemo waandaaji, washiriki pamoja na wadhamini wetu kwa kufanikisha lengo hili muhimu. Pamoja na kwamba tumepata washindi wa mbio hizi lakini bado kila mshiriki ni mshindi kwasababu amefanikisha kuokoa maisha ya mama zetu,’’ alisema.
Akipokea msaada huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Julius Mwaiselage aliishukuru benki hiyo kwa jitihada hizo huku akibaisha kuwa msaada huo unakwenda kusaidia mapambano hayo katika maeneo mbalimbali hususani mikoani ili kuwahi matibabu kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakifika hospitalini wakiwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa huo.
Awali akizungumzia matokeo hayo Rais wa Shirikisho la Riadha Taifa (RT) Bw. Silas Isangi alisema kufanya vizuri kwa watanzania katika mbio mbalimbali hapa nchini ni kutokana na maandalizi mazuri yanayofanywa na wanariadha hao huku akibainisha kuwa huo ni mwanzo tu kwa kuwa matokeo hayo mazuri ya watanzania yanatarajiwa hadi kimataifa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.