WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji, biashara na kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Mpaka sasa, hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo tarehe Juni 27, 2019 jijini Dodoma alipokuwa akifungua Kongamano la Uwekezaji la Mkoa wa Dodoma kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
”Miongoni mwa hatua hizo ni uwepo wa usafiri wa uhakika na wa haraka kwa abiria na mizigo kwa kujenga Reli ya Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway)”. Waziri Mkuu aliongeza kuwa uwanja wa ndege wa Dodoma umeboreshwa na kuruhusu ndege kubwa na ndogo kutua wakati wowote. ”Mashirika ya ndege yanayotoa huduma yameongezeka na maandalizi ya awali ya ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege katika eneo la Msalato yanaendelea”.
Aidha, Waziri Mkuu amesema mkoa wa Dodoma una barabara za kuaminika za kiwango cha lami zinazoiunganisha mikoa mingine ya jirani hadi na nchi jirani.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha huduma za afya na Dodoma kuna hospitali ya Benjamin Mkapa yenye uwezo kama wa Muhimbili na Mloganzila. Na hata Hospitali ya Rufaa ya Dodoma imeongezewa vifaa vya kisasa na madaktari mabingwa ili kuimarisha utoaji huduma za afya zilizo bora.
Amesema ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji ‘Stiegler’s Gorge’ wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115, utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini pamoja na kuwa kiasi cha umeme kinachopatikana sasa kinatosheleza na kubaki na umeme wa ziada.
“Mradi huo utaongeza upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya viwanda na uwekezaji nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo mkoa wa Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa mpango wa Kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji (The Blue Print) utakaoanza Julai mosi mwaka huu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema anatarajia kuwa kongamano hilo litawezesha kupatikana kwa wawekezaji mahiri kwa maendeleo ya uchumi na wananchi wa Tanzania.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge alisema katika azma ya Selikali ya kujenga uchumi wa viwanda wameandaa kongamano hilo ili kutangaza fursa zilizopo katika mkoa wa Dodoma, wilaya zote na Jiji la Dodoma.
Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Dodoma Fursa Mpya Kiuchumi Tanzania, Wekeza Dodoma Tukufanikishe’, inaweka wazi nafasi ya mkoa wa Dodoma kwa sasa na baadaye.
Dkt. Mahenge alitaja baadhi ya fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Dodoma kuwa ni pamoja na uwepo wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, viwanda na taasisi afya, elimu, bila kusahau hali ya usalama na amani ziivyopo sasa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.