MIKOA ya Dodoma na Singida imetakiwa kuweka utaratibu wa kuvuma maji ya mvua ili yatumike katika shughuli za kilimo na kupunguza utegemezi wa mvua.
Kauli hiyo ilitolewa na mgeni rasmi katika kilele cha maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, Canon Dkt Rehema Nchimbi alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma hivi karibuni.
Canon Dkt Nchimbi ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida alisema kuwa shughuli za kilimo na mifugo katika mikoa hiyo zinategemea sana mvua. “Mvua ikikosekana shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi utayumba na malisho yatapotea kabisa. Kupitia Nanenane hii tutote na suluhisho. Tanzania tuna ardhi ya kutosha kubeba kilimo na mifugo. Haiwezekani tuwe mikoa kame, mikoa masikini, mikoa ya njaa. Tukatae kabisa umasikini” alisema Canon Dkt Nchimbi.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa ni Mkoa wa Dodoma pekee ambapo zabibu zinalimwa mara mbili kwa mwaka. “Ni korosho za Singida zinazolimwa mara mbili kwa mwaka, ni alizeti ya Singida inayozaa mara mbili kwa mwaka. Dodoma na Singida siyo kame, Dodoma na Singida siyo masikini, Dodoma na Singida hakuna njaa. Tutaondoa ukame kwa mipango. Tuweke utaratibu wa kuvuma maji ya mvua. Tuzo zijazo za Nanenane tutenge zawadi kwa watakaoonesha ubingwa katika kuvuna maji ya mvua. Na tuzo kwa mkulima bora malisho ya mifugo” alisema Canon Dkt Nchimbi.
Maonesho ya 26 ya Nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Nanenane Nzuguni Dodoma yalishirikisha makampuni 36, wajasiriamali 300 na taasisi 43 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Kilimo, mifugo na uvuvi kwa ukuaji wa uchumi wa nchi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.