HALMASHAURI za Mkoa wa Dodoma zimetakiwa kuhakikisha zinafikia asilimia 80 ya shule zinazotoa chakula kwa wanafunzi wakati wa masomo. Hayo yameelezwa leo Februari pili, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa kikao cha lishe cha robo ya pili ya mwaka (Oktoba - Desemba 2023) kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kikao hicho kimejikita kujadili umuhimu wa upatikanaji wa chakula shuleni pamoja na mikakati ya kuboresha huduma hiyo kwani chakula ni nguzo muhimu ya kusaidia kuinua taaluma na kutatua changamoto ya utoro hasa kipindi hiki ambacho Mkoa umeweka mkakati wa kuinua Elimu.
Senyamule amesema Mkoa umepiga hatua kwenye utekelezaji wa afua za lishe kwani lishe ndio jambo pekee lililosainiwa mikataba ya utekelezaji wake na Serikali.
"Mkoa wetu umeonesha matokeo mazuri kwa kipindi cha miezi 6 ya mwanzo wa mwaka 2023. Tumefikia 100.18% ya utekelezaji wa afua za lishe ambazo ni pamoja na 99.9% utoaji wa madini ya chuma kwa mama wajawazito, 100% matibabu ya utapiamlo, 101% unasihi kwenye ulishaji, 99.8% kwenye lishe, 105.3% utoaji wa vitamin A pamoja na 100% vikao vya lishe.
"Mpaka Sasa shule zinazotoa chakula ni 99% ingawa wanaotekeleza agizo hilo ni 64% tu. Tujiwekee mkakati angalau tufikie 75%. Viongozi muende mukalifanyie kazi kwa umakini kabisa hadi kufikia Juni 2024 tukamilishe. Mafanikio haya ni kutokana na ushirikiano wa Serikali na wadau hawa." Amesema Mhe. Senyamule.
Aidha, kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wanaotekeleza miradi ya lishe kwenye Halmashauri za Mkoa wa Dodoma ambao ni Save the Children wanaotekeleza mradi wa 'Lishe yangu, maisha yangu', World Vision Tanzania, USAID, Sanku, Action against Hunger pamoja na Cuham ambapo miradi yao inajikita katika kupunguza utapiamlo kwa kusaidia upatikanaji wa chakula cha kutosha.
Hata hivyo, wakati wa kikao hicho, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Bestie Magoma, ametumia kikao hicho kutoa taarifa ya maandalizi ya kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Surua itakayoanza Februari 15 hadi 18, 2024 ambapo maandalizi ya awali yanaendelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.