MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema, uongozi wa Mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa unaondoa urasimu pamoja na kuboresha mazingira rafiki na salama ya kufanya uwekezaji.
Akiongea mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili cha Itracom kinachojengwa katika eneo la Nala nje kidogo ya Jiji la Dodoma, Mtaka amesema lazima wahakikishe urasimu wote unaondolewa ili kuwepo na mazingira bora ya kuwekeza.
"Tutakapoondoa urasimu tutapata wawekezaji na hawa watu watatusaidia kama hivi vijana wetu wanapata ajira lakini pamoja na kupata ajira muwajali wakiwa kazini uwape vitendea kazi na kauli nzuri wawapo kazini" amesema Mtaka.
Aidha, amekemea tabia ya wawekezaji kuondoa wafanyakazi wanaowasilisha mawazo yao na kutaja hatua hiyo kuwa haikubaliki katika sheria ya Tanzania, huku akiweka msisitizo kile alichokitaja kama ni Watanzania kupewa kipaumbele katika ajira na si watu wengine.
Mtaka ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kuweka usawa katika kazi kwa wazawa kwani katika kiwanda hicho kumeonekana kuwepo na idadi kubwa ya watu kutoka Burundi kuliko Tanzania.
Kwa upande wake Emmanuel Mavunde mfanyakazi katika kiwanda hicho amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwa na wasiwasi wa kufukuzwa kazi hasa pale wanapohoji jambo huku wakitupiwa kauli ambazo si rafiki na posho pia ni ndogo ikilinganishwa na kazi wanazofanya.
Awali muwakilishi wa Intracom Tanzania, Bwana Samson Rubenga alisema watahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kiwanda kinafikia lengo.
Hata hivyo kiwanda hicho kinatarajia kukamilika Juni, 2022 ambapo kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea tani laki 6 huku wananchi elfu 3 wakipata ajira ya kudumu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.