SERIKALI ya Mkoa wa Dodoma imeomba maonesho ya Nanenane kitaifa mwaka 2021 yafanyike katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuipa heshima Makao Makuu ya nchi na fursa kwa wananchi wengi kujionea maarifa yatokanayo na maonesho hayo katika kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi.
Ombi hilo lilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akiongea na wannanchi katika maonesho ya Nanenane kwenye uwanja wa Nanenane Nzuguni jijini hapa.
Dkt. Mahenge alisema “nikuombe Mheshimiwa Waziri, Dodoma ni Makao Makuu yetu sote na itajengwa na watanzania wote. Namna moja wapo ya kujenga na kuharakisha ustawi wa Makao Makuu ni pamoja na mchango wa kufanyia shughuli mbalimbali za kitaifa Makao Makuu. Tumeshuhudia sherehe za Uhuru zikifanyikia hapa, tumeshuhudia sherehe za Muungano zikifanyikia hapa, itapendeza sana Mheshimiwa Waziri ukitupelekea maombi kwamba na sherehe hizi za Nanenane za kitaifa ziweze kufanyikia Makao Makuu hii itatangaza sana na kuleta wawekezaji katika Mkoa wetu na Makao Makuu ya nchi”.
Akiongelea maonesho yanayoendelea kwenye uwanja wa Nanenane, aliwashawishi wananchi wengi kutembelea maonesho hayo ili kunufaika na maonesho hayo. “Katika maonesho haya hasa kwenye mabanda, kuna vitu vingi vinaoneshwa ambavyo ni fursa kwenu wana Dodoma ambao tupo karibu kuliko mikoa yote kwenda kuyaona. Na kama tunataka kumuunga mkono Mheshimiwa Rais lazima tuanze kuzalisha kwa nguvu zetu zote na kwa wingi ili tuweze kunufaika na miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu” alisema Dkt. Mahenge.
Aidha, aliwashukuru wadau wote waliochukua maeneo kwa ajili ya kuonesha shughuli zao katika Nanenane.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.