WILAYA ya Dodoma imepongezwa kwa kupiga hatua kimaendeleo kufuatia ujenzi wa miundombinu inayoboresha maisha ya wananchi na huduma bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge maalum wa Uhuru kitaifa, Lt. Josephine Mwambashi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kuulaki Mwenge Maalum wa Uhuru ulipoenda kuzindua barabara ya lami ya Kikuyu-Chidachi-Kinyambwa-Itega yenye urefu wa kilometa 6.05.
Lt. Mwambashi alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara unalenga kuwezesha kupata huduma muhimu kwa haraka. “Barabara hii ni muhimu kwa sababu imesaidia kupunguza tatizo la kujaa maji katika eneo la shule na maeneo mengine kutokana na ujenzi wake na mifereji. Dodoma inaendelea sana, tofauti na miaka ya nyuma” alisema Lt. Mwambashi.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara pembezoni mwa barabara kufanya usafi ili kutunza miundombinu hiyo na mazingira.
Baada ya kutembelea na kukagua barabara hiyo kisha kukagua na kujiridhisha na nyaraka, Kiongozi wa mbio za Mwenge Maalum wa Uhuru alizindua barabara hiyo.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kikuyu-Chidachi-Kinyambwa-Itega, Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mhandisi Emmanuel Manyanga alisema kuwa lengo la ujenzi wa barabara hiyo lilikuwa kuboresha miundombinu ya mji. Lengo lingine ni kuwezesha mawasiliano baina ya wakazi wa eneo moja na lingine.
Kuhusu gharama za mradi huo, alisema kuwa asilimia 98.59 ililipwa. “Mpaka kufikia mwisho wa utekelezaji, Mkandarasi M/S Stecol Corporation kutoka China alilipwa shilingi 9,280,998,492.73 sawa ma asilimia 98.59 ya bajeti iliyotengwa” alisema Mhandisi Manyanga.
Mradi wa barabara hiyo ni sehemu ya Mradi wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati (TSCP) uliofadhiliwa na Serikali kuu kupitia mkopo wa Benki ya Dunia.
Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2021 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.