Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge leo amezindua rasmi Mkakati wa kutokomeza mbu na wadudu wadhulifu katika mkoa wa Dodoma na kusisitiza kuwa mafanikio ya kiuchumi wa nchi yetu yanategemea sana wananchi kuwa na afya bora kwa kuepukana na maradhi.
Dkt. Mahenge ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi huo wa kimkoa uliofanyika Jijini Dodoma, kata ya Mnadani kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mnadani mbele ya mkutano mkubwa wa wananchi waliojitokeza tangu mapema asubuhi saa 12:30 ambapo shughuli hii ilianza kwa kufanya usafi eneo lote la shule ya Mnadani na mitaa inayozunguka shule hiyo.
Wakati tunapata Uhuru, Mwalimu Nyerere aliwatangaza maadui wakubwa wa nchi hii kuwa ni Ujinga, Umaskini na Maradhi, hata leo bado tunapambana na adui maradhi. Aliongeza kuwa Tanzania hatuwezi kujenga uchumi imara wa nchi yetu kama tunatendelea kuwa na changamoto ya maradhi kwa wananchi wetu. Alisema Mkuu wa Mkoa.
Kwa misingi hii, Rais wetu Dkt. John Magufuli wakati akiomba kula mwaka 2015 aliliona hili na kusisitiza kuwa endapo wananchi wanampa ridhaa ya kuiongoza nchi yetu, miongoni mwa mambo atakayoyashughulikia na kuyapa kipaumbele ni kujenga miundombinu ya huduma za Afya na kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba. Akifafanua zaidi Dkt. Mahenge alisema kuwa, katika Mkoa wa Dodoma Serikali imejenga vituo vya Afya 21, na serikali pia imeongeza bajeti ya Afya kutoka shilingi milioni 900 hadi kufikia bajeti ya shilingi bilioni 4 kwa mwaka. Pia katika kipindi cha miaka mitatu ambacho serikali imekaa madarakani, tayari Hospitali 3 za Wilaya zimeanza kujengwa katika Wilaya za Chemba, Bahi na Chamwino, lakini pia Mhe. Rais aliamuru kujengwa kwa Hospitali ya Uhuru katika mkoa wa Dodoma kwa kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia sherehe za maadhimisho ya Uhuru.
Mahenge akakumbusha juu ya jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanya na serikali kwa kuanzisha kampeni za kupambana na maradhi kama vile kampeni ya Jitambue, kampeni ya kupambana na maambukizi ya UKIMWI/VVU, kampeni ya kupambana na Maralia, kampeni ya Lishe na kadharika. Zote zikilenga kuimarisha afya za wananchi kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao na nchi kwa ujumla. Hivyo akasisitiza kuwa kila mwananchi wa Dodoma pamoja na zoezi la kupiga dawa ya kuua mbu na wadudu wadhulifu, ni lazima kuhakikisha kila mmoja anafanya usafi nyumbani kwake, barabani na maeneo ya biashara ili kutokomeza uchafu na mazalia ya mbu kwenye maeneo yetu yanayotuzunguka kiasi cha mita tano.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alilipongeza Jiji la Dodoma na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kwa kufanya maandalizi ya uzinduzi wa mkakati wa kutokomeza mbu na wadudu wadhulifu mkoani Dodoma. Katika kusisitiza na kuwaelekeza watendaji wa Wilaya kutekeleza hili, Dkt. Mahenge aliwagawia Wakuu wa Wilaya wote wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma kitabu chenye mkakati wa kutokomeza mbu na wadudu wadhulifu ili wakasimamie mkakati huo katika maeneo yao ya kazi. Waliopewa ni wakuu wa Wilaya za Dodoma Mjini, Mpwapwa, Kongwa, Chamwino, Chemba, Kondoa na Bahi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.