SERIKALI ya Tanzania imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa Sh trilioni 1.14 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu ya maendeleo.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma na ujenzi wa Daraja kwenye Kivuko cha Mto Pangani.
Hayo yamebainika jana jijini Dar es Salaam wakati wa kutiwa saini kwa mikataba hiyo, kulikofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James na Mwakilishi Mkazi wa AfDB nchini, Dk Alex Mubiru.
Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, James alisema fedha hizo Shilingi trilioni 1.14 ni sawa na Dola za Marekani milioni 495.59, ambazo zimegawanywa kwenye miradi mitatu.
Alitaka miradi hiyo na kiasi cha fedha kitakachotumika kuwa ni Dola za Marekani milioni 271.63 zitatumika kwenye utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, Dodoma, ambapo maandalizi ya mradi huo yameanza.
Akizungumzia mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale alisema katika fedha hizo za AfDB, Dola za Marekani milioni 271.63 zimetengwa kuufanikisha ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 757.78, huku pia serikali ikichangia fedha za ndani Sh bilioni 133.03 sawa na asilimia 17 ya fedha zote.
Mfugale alisema mradi huo wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato utakaohudumia watu milioni 1.5, utahusisha barabara za kukimbilia ndege na ujenzi wa majengo ya abiria ya kisasa.
“Uwanja wa Msalato utakuwa uwanja wa kisasa mkubwa, wenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 1.5 kwa wakati mmoja, uwanja utakuwa na urefu wa Kilomita 3.6 utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner 17 na Airbus 380 kwa wakati mmoja,”alisema Mfugale.
Alisema hivi sasa mchakato wa kumpata mkandarasi umeshaanza, kwani zabuni ilifunguliwa Februari 13 mwaka huu na itafungwa Aprili 19, mwaka huu. Kwamba katika kutekeleza mradi huo, Sh bilioni 15.42 zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wale watakaopaswa kuondoka kupisha mradi.
Kuhusu mradi wa pili utakaonufaika na fedha hizo za AfDB, James alisema ni Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo- Horohoro/Lungalunga-Malindi na Ujenzi wa Daraja kwenye Mto Pangani, mradi unaotekelezwa kwa kiwango cha lami.
Mradi huo umetengewa Dola za Marekani milioni 168.76, ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 448.6, huku huku pia serikali ikichangia Sh bilioni 58.473 sawa na asilimia 13.33 ya fedha zote .
Akifafanua mradi huo, Mfugale alisema katika utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa barabara na daraja hilo, fidia ya Sh bilioni 10.3 imetengwa kwa watakaopaswa kuondoka, kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Aidha, mradi wa tatu uliopata fedha za AfDB jana ni Programu ya Utawala Bora na Kuendeleza Sekta Binafsi, ambapo umetengewa Dola za Marekani Milioni 55.2 Mwakilishi Mkazi wa AfDB nchini, Dk Alex Mubiru alisema fedha hizo zitasaidia kuimarisha maisha ya watu, kwa kuhakikisha miradi ya maendeleo itatekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija kwa taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elius Mwakalinga alimshukuru Rais Johm Magufuli kwa kudumisha uhusiano nzuri baina ya wadau hao, ambao wamefanikisha utekelezaji wa miradi mingi nchini, ambayo hadi sasa inafikia Dola za Marekani bilioni 2.1.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kushoto), akisaini Mikataba mitano yenye thamani ya Dola za Marekani 495.59 na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Alex Mubiru (kulia) katika hafla iliyofanyika Benki Kuu Jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu Tanroad, Patrick Mfugale akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege wa Kimaifa wa Msalato Jijini Dodoma, Ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo-Pangani-Tanga uliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam.
Chanzo: habarileo.co.tz
Tazama pia:- AfDB imeipatia Tanzania Mkopo wa Masharti Nafuu US Dola Milioni 495.59
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.