Wananchi wa Jiji la Dodoma wametakiwa kujali afya zao kwa kujiunga na Bima ya bei nafuu ya CHF iliyoboreshwa inayopatikana kwa gharama ya shilingi elfu thelathini (30,000/=) kwa watu sita, ili kujihakikishia matibabu katika vituo vyote vya afya vya Serikali wakati wowote wanapougua.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa CHF Jiji la Dodoma Patrick Sebiga wakati timu ya Maafisa uandikishaji ilipokua ikitoa huduma ya kugawa kadi hizo za matibabu katika eneo la Nyerere Square ambapo idadi kubwa ya wakazi wa Dodoma wamejitokeza kwa wingi kuchukua kadi hizo.
Sebiga amesema kuwa Mfuko wa Afya ya Jamii wa CHF iliyoboreshwa, ni mpango wa hiari ulioanzishwa kwa ajili ya Kaya, Familia, Kikundi au mtu binafsi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua.
“Bima hii ni nafuu sana, unachangia elfu thelathini (30,000/=) tu kwa watu sita ambapo mnatibiwa mwaka mzima katika Zahanati, vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya nchi nzima, Bima hii inakuwezesha kufanyiwa mpaka upasuaji mdogo, hivyo tunawahimiza Watanzania wote kujitokeza kwa wingi kuchukua Bima hii nafuu” – Alisema Sebiga.
Akizungumzia faida za Bima hiyo Sebiga alisema kuwa mgonjwa atapata huduma ya matibabu ya kutwa na kulazwa kwa mujibu wa mwongozo wa Wizara ya Afya, Vipimo vya Maabara, Afya ya mama na mtoto Pamoja na huduma ya Dawa kulingana na ushauri wa Daktari.
“Bima ya afya ya CHF Iliyoboreshwa inatolewa na maafisa waandikishaji wanaopatikana katika ofisi za Jiji zilizopo karibu na Sabasaba (zilipokuwa ofisi za Manispaa zamani) chumba namba tatu, lakini pia wapo Nyerere Square pamoja na Soko la Bonanza. Unatakiwa ufike ukiwa na picha (passport size) za watu wote sita wanaowajumuika katika bima, majina yao na miaka yao ya kuzaliwa bila kusahau shilingi elfu thelathini (30,000/=) na utakabidhiwa kadi sita, yaani kila mwana familia atakua na kadi yake” Aliongeza Sebiga.
Afisa Mwandikishaji wa CHF iliyoboreshwa Maggie Owino akitoa elimu kwa mwendesha bodabod
Mratibu wa CHF iliyoboreshwa wa Jiji la Dodoma Patrick Sebiga akimwandikisha mmoja wa wananchi waliojitokeza kujisajiri na Mfumo wa CHF iliyoboreshwa.
Khadija Seif ambaye ni Afisa Mwandikishaji wa CHF iliyoboreshwa akiwaandikisha mama pamoja na mwanae kuwa wanufaika wa mfuko wa CHF.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.