TAASISI mbalimbali na watu binafsi, wameonesha nia ya kumsaidia mwanafunzi, Yonana Lugedenga pamoja na familia yake, kumwezesha aendelee na masomo yake, baada ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, licha ya mazingira magumu aliyosomea.
Aidha, upande wa serikali, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mwanafunzi huyo ambaye ni tunda la mafanikio ya sera ya elimu bure, atapewa Sh milioni moja na kununuliwa vifaa vinavyohitajika, kujiunga na kidato cha tano, kama ilivyo kwenye mpango uliofikiwa na mkoa. Hata hivyo, Mtaka alisema jana kutokana na maoni na hoja mbalimbali, zilizotolewa kuhusu mwanafunzi huyo, katika tathimini watakayoifanya, wataangalia uwezekano wa kuweka pia mpango wa kufuatilia na kuwezesha wanafunzi wanaofaulu hadi chuo kikuu.
Yohana ambaye amehitimu Shule ya Sekondari ya Igaganulwa Kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, amefaulu mtihani wa kidato cha nne kwa kupata alama A masomo yote tisa. Mtaka alisema miongoni mwa taasisi ambazo zimewasiliana naye, zikitaka kumsaidia mtoto huyo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lililosema linataka kumsaidia.
“Unesco wamenipigia simu, nadhani wanataka kum-support. Wana nia hata ya kusaidia wadogo zake…” alisema na kuongeza kuwa pia mkurugenzi mtendaji wa benki ya NMB na watu binafsi, waliowasiliana naye, walionesha kuwa wana jambo wanataka kulifanya.
Akizungumzia matokeo na mjadala ulioibuka, kuhusu ufaulu wa Yohana aliyekuwa akisoma shule ya kata ya Igaganulwa, Mtaka alisema ni uthibitisho wa umma, kuanza kuamini shule za serikali.
Alisema jambo ambalo umma haujafahamishwa ni kwamba mwanafunzi huyo, anamulika mafanikio ya sera ya elimu bure, iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli.
“Hii ndiyo Form Four (kidato cha nne) ya kwanza tangu Rais Magufuli aingie madarakani. Kama isingekuwa elimu bure huyu mtoto angewezaje kusoma? Maeneo kama haya (vijijini) maisha yalikuwa magumu. Hata huyu mtoto asingeweza kusoma,” alisema Mtaka.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akimzungumzia kijana huyo alisema “Inatia hamasa sana na kumshukuru sana Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Magufuli kwa kuleta elimu bure. Maana taarifa ni kwamba kijana huyu hata uniform (sare) za shule kwa miaka yote alikuwa ananunuliwa na walimu wake kwa vile alijulikana kwa kuwa na akili nyingi sana”.
Kulingana na mkakati wa mkoa, kuhusu watoto wa shule za serikali wanaofaulu kwa kupata alama 7 kwa maana ya A katika masomo yote kidato cha nne, hupewa Sh milioni moja za kukidhi mahitaji yake. Vivyo hivyo, kwa kidato cha sita kwa mwenye ufaulu wa alama 3.
Kwa mujibu wa Mtaka, mwaka jana pia mkoa wa Simiyu ulipata mwanafunzi aliyefaulu kwa alama 7 kutoka shule ya serikali. Alitoka Shule ya Sekondari ya kata ya Nkololo wilayani Bariadi. Akizungumzia kambi za kitaaluma, Mkuu wa Mkoa alisema zimekuwa na faida kubwa.
Alisema mwaka 2016 alipofika Simiyu, katika mitihani yote ya kitaifa; darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na sita, mkoa ulikuwa ukishika nafasi za 26,25 na 22.
“Lakini leo katika mitihani yote, mkoa umeingia kumi bora. Utaona mwaka 2016 katika kidato cha nne tulikuwa wa 22, mwaka 2017 wa 14, mwaka 2018 wa tisa na mwaka 2019 tukawa wa tano. Wakati huo huo katika Darasala la Saba mwaka 2018 tulikuwa wa 22, mwaka 2019 namba tisa,” alisema Mtaka.
Kwa mujibu wa Mtaka, mwaka jana, katika matokeo kwa shule za serikali, Simiyu iliingiza watoto wanne katika 10 bora na shule moja katika shule 10 bora. Mtaka alisema jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na serikali ni kutafuta namna ya kusaidia watoto, kuondokana na kusafiri umbali mrefu kwenda shule.
Chanzo: habarileo.go.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.