Na. Mussa Richard, DODOMA
Timu ya Mpira wa Miguu ya Elimu Kombaini imeishushia kipigo cha mbwa mwizi Timu ya Mpira wa Miguu ya Sheria ndogo FC baada ya kuichabanga mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma ikiwa ni muendelezo wa michezo mbalimbali katika tamasha la kuukaribisha Mwaka 2025 la CCD Watumishi Bonanza lililoandaliwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma.
Baada ya mchezo kutamatika Nahodha wa timu ya Elimu Kombaini, Given Alestides, alisema “tumefanikiwa kupata matokeo na tukiwa kama watu wa elimu tumewafundisha wanasheria jinsi ya kucheza mpira wa miguu na wameelewa, lakini yote kwa yote tumefurahi kushiriki bonanza hili na tumekutana wa watu wengi na tumejifunza mambo mengi sana, tunampongeza sana Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa ubunifu huu alioufanya”.
Nae Nahodha wa Timu ya Sheria ndogo, Salumu Bwenda akatoa sababu zilizowafanya wapoteze mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao. “Mchezo umeisha na tumepoteza kwa bao 3-1 ni matokeo mabaya lakini sababu kubwa ni kuwa wachezaji wetu wana maumbo makubwa na umri umeenda pia ndiyo maana hata magoli mengi tuliyofungwa yalitokana na wapinzani wetu kupiga mipira mirefu nyuma ya mabeki na kukimbia kwa kasi kuingia kwenye boksi letu, yote kwa yote naamini watu wote wamefurahia mpira kwasababu hii ilikua ni burudani na ni moja ya mazoezi” alisema Bwenda.
Bonanza hilo lililoandaliwa lilikuwa na lengo la kuwakutanisha watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuukaribisha Mwaka 2025 huku kaulimbiu kwa mwaka huu ikiwa ni ‘Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ushirikiano na Umoja Wetu Ndiyo Nyenzo ya Huduma Bora’.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.