Na. Coletha Charles, IPAGALA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea na jitihada ya utambuzi wa watoto wenye mahitaji maalum kiafya kwa lengo la kujiunga na elimu ya awali na msingi kwa mwaka wa masomo 2025 katika Kata ya Ipagala.
Akizungumza wakati zoezi hilo, Afisa Elimu wa Kata ya Ipagala, Veronica Mpanda, aliwaomba wazazi kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum shule kwa sababu wanahaki ya kupata elimu kama watoto wengine kulingana na sera ya elimu jumuishi kwa kuwa miundombinu imara ipo kwa ajili yao.
Alisema kuwa zoezi hilo linalenga kutambua idadi na aina ya mahitaji ya watoto hao ili kuweka mipango madhubuti ya kuwahudumia. “Zoezi hili la uandikishaji lilitakiwa lifanyike katika Shule ya Msingi ya Ipagala B, lakini hatujafanikiwa kupata mtoto hata mmoja mwenye mahitaji maalum japo zoezi hili ni endelevu na tunatambua kwamba elimu ni haki ya kila mtoto na kupitia zoezi hili tutahakikisha kuwa hakuna mtoto anayebaki nyuma kwa sababu ya changamoto yoyote” alisema Mpanda.
Nae, Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Upimaji Shule ya Msingi Nkuhungu, Deogratias Montano, alisema kuwa wanawapima na kuwapangia watoto hao shule stahiki ambazo wanaweza kusoma bila shida na zoezi hilo litaendelea ndani ya wiki mbili.
Alisema kuwa mwitikio bado siyo mzuri kwa wazazi na walezi wa watoto wenye mahitaji maalum japokuwa wamejipanga kutokuacha mtoto nyumbani ambaye ana ulemavu wa macho, ulemavu wa viungo, mtindio wa ubongo na ulemavu wowote. “Tunashirikiana kwa karibu na wazazi na walezi wa watoto hawa ili kuhakikisha tunapata taarifa sahihi. Hii inatusaidia kupanga huduma zinazofaa kulingana na mahitaji ya kila mtoto na hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya jamii nzima. Elimu inatakiwa itolewe kwa upana juu ya jamii kuhusu umuhimu wa kuwasaidia watoto” alisema Montano.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejipanga kuboresha hali ya watoto wenye mahitaji maalum kwa kuhakikisha wanajumuishwa kikamilifu katika mfumo wa elimu na maisha ya kila siku.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.