NA. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupeleka timu ya hamasa na elimu juu ya Anuani za Makazi Kata ya Mbabala ili kufanikisha zoezi hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akijibu swali la Diwani wa Kata ya Mbabala, Mheshimiwa Paskazia Mayala (pichani juu) aliyetaka kujua lini kata yake itapata uhamasishaji wa anuani za makazi ili wananchi wachangamkie fursa hiyo ya kupata namba za makazi katika nyumba zao. Mheshimiwa Mayala aliuliza katika mkutano wa Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkurugenzi Mafuru alifafanua kuwa elimu ya Anuani za Makazi ilitolewa kwenye ngazi zote katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tulipeleka waratibu kwenda kujifunza Morogoro. Waliporudi tukatoa elimu katika ngazi ya jiji, watendaji na wenyeviti wa mitaa. Lengo lilikuwa kujua nani anaendesha zoezi hilo na taratibu zake zilivyo ili kuwa na uelewa wa pamoja” alisema Mafuru.
Akiongelea wataalam kwenda tena Kata ya Mbabala, alisema kuwa watakwenda kesho. “Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kuwa kesho wataalam wa Anuani za Makazi watafika Kata ya Mbabala na kufanya uhamasishaji. Sasa hivi wanarudia kuhakikisha maeneo ambayo hawakufanya vizuri. Mimi naangalia taarifa za kila siku za mwenendo wa zoezi hili. Kesho watakuwepo Mbabala na kazi itafanyika kwa kiwango cha juu” alisema Mafuru kwa kujiamini.
Zoezi la uandikishaji Anuani za Makazi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma limefikia asilimia 86.85.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akipokuwa akijibu swali za Mheshimiwa Diwani Paskazia Mayala wa Kata ya Mbabala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.