HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Action for Community Care wametoa mafunzo ya jinsi ya kutengeneza vitalu vya miti kwa Walimu na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Gawaye iliyopo katika Kata ya Chihanga Jijini hapa, ikiwa ni katika harakati za kuendeleza na kuunga mkono kampeni ya Dodoma ya kijani.
Akizungumza na Mwandishi wetu, Mkurugenzi wa Shirika hilo Pendo Maiseli amesema kuwa lengo kuu la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Walimu na Wanafunzi ili wawe sehemu ya kampeni ya Dodoma ya kijani ili wawe mabalozi wazuri wa kampeni hiyo.
Maiseli amesema kuwa Watoto wanapofundishwa inakua ni rahisi kushika na wanaamini baada ya kushika watahamishia mafunzo hayo nyumbani hivyo mafunzo hayo yatakua yameifikia jamii kubwa kupitia kwa wanafunzi hao.
“Tunaamini baada ya muda fulani eneo hili litakua la kijani kwa sababu wanafunzi tuliowapatia mafunzo haya wataenda kuzifundisha familia zao hivyo sehemu kubwa ya mji huu itakua ya kijani.” Aliongeza Maiseli.
Kwa upande wake Afisa Misitu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Bakari Maluma, amelishukuru Shirika hilo kwa kufadhili zoezi la utoaji wa mafunzo hayo yatakayosaidia jamii ya eneo hilo kuandaa vitalu vya miti ambayo baadae wataipanda na kuondokana na hali ya ukame katika maeneo yao.
Maluma amesema kuwa wameamua kutumia Shule kwasababu wanaamini kupitia wanafunzi watazalisha miche mingi ambayo itasaidia kukijanisha eneo hilo na Dodoma kwa ujumla.
“Niwashukuru sana Action for Community Care kwa msaada wao kwasababu tumekua tukishirikiana sana katika masuala mbalimbali yanayohusu Mazingira, niwaombe na wadau wengine wajitokeze ili tuweke Jiji letu hatika hali ya ukijani” Aliongeza Maluma.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwl. Magaeli Komkoi amesema licha ya kupewa elimu hiyo, pia Shirika hilo limewapatia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kutunza Mazingira.
Mwl. Komkoi ameongeza kuwa watahakikisha wanatengeneza kitalu kikubwa cha miti na kukitunza vizuri ili shule hiyo iwe ya mfano kwa upandaji na utunzaji wa miti ambapo watapanda miti ya matunda na vivuli ambayo wataitumia kwa kupata matunda na kupumzika.
Picha na matukio mbalimbali wakati wa mafunzo
Maelekezo ya jinsi ya kuchanganya udongo na mbolea wakati ya matayarisho ya kitalu.
Mwanafunzi akifanya mafunzo kwa vitendo.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Action for Community Care hilo Pendo Maiseli
Maiseli akiwaonesha wanafunzi kwa vitendo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.