ENEO la Bahi Road lililopo Kata ya Kizota ambalo limetengwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabishara wadogo maarufu kama machinga limeanza kufanyiwa usanifu na Jiji hilo kwa kushirikiana na Chuo cha Ardhi ili liwe rafiki kwa kuwekewa miundombinu muhimu tayari kwa kuwahamishia wafanyabiashara hao.
Meya wa Jiji hilo Mstahiki Prof. Davis Mwamfupe alifika katika eneo hilo mapema leo Novemba 4, 2021 na kushuhudia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa na vibanda na wauza mbao wakibomoa na kuondoa bidhaa zao ili kupisha kazi ya kuliandaa eneo hilo kitalaam huku likitarajiwa kuwekewa sakafu ya mawe na taa ili kuwezesha biashara kufanyika hata wakati wa siku.
Baadhi ya washafanyabiashara waliokuwa wakibomoa vibanda vyao kwa hiyari yao walikiri mbele Meya Mwamfupe kuwa wameshirikishwa vizuri na Jiji katika zoezi la kupisha eneo hilo na hakuna nguvu ya ziada iliyotumika zaidi ya mazungumzo ya pande mbili na ndiyo sababu wanabomoa vibanda vyao vya awali na kuhamisha bidhaa.
Hivi karibuni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru aliliambia Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kuwa, baada ya maelekezo ya Serikali kuhusu kuwapanga kwa utaratibu mzuri wafanyabiashara hao, Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa na Chuo cha Ardhi walikagua maeneo saba tofauti ili kupata eneo zuri zaidi la wafanyabiashara hao kuhamia kwa ajili ya shughuli zao.
Mafuru alikuwa akijibu swali la papo kwa papo la diwani wa Kata ya Nkuhungu Mhe. Daudi Mkhandi aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na Halmashauri ya Jiji kuhusu suala kuwapanga wamachinga baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa agizo la kupangwa vizuri kwa wafanyabiashara hao bila kuathiri shughuli zao.
Mkurugenzi Mafuru alisema eneo la 'Bahi road' ni muafaka kwa wafanyabiashara hao na kwamba walishafanya nao kikao na kwamba Halmashauri itaweka sakafu ya mawe katika eneo hilo na kujenga vibanda vidogo ambavyo vitatumiwa kuwekea bidhaa za wafanyabiashara hao.
“Mheshimiwa mwenyekiti, baada ya agizo la Mhe. Rais sisi hatukutaka kuwaswaga tu wamachinga bali tunataka kuwaboreshea mazingira ya kazi zao kwa kuwaandalia eneo zuri sana pale 'Bahi road', eneo lile lina uwezo wa kuchukua zaidi ya machinga 2,000 na sisi jiji la Dodoma tuna takribani machinga 1950” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Alisema Jiji limekuja na mpango wa kushirikiana na wataalam wa Chuo cha Ardhi ili watengeneze mazingira ya kisasa ya eneo la kibiashara ili pia kuupendezesha mji na kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara hao na tayari kazi imeshaanza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.