WAWEKEZAJI wa ndani na nje ya nchi wamealikwa kuwekeza katika eneo lenye ukubwa wa hekta 507 kwa ajili ya bandari kavu na maghala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwaliko huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alipofanya wasilisho juu ya fursa ya uwekezaji katika bandari kavu kwenye kongamano la uwekezaji lililofanyika katika ukumbi wa ‘Dodoma Convention Centre’, jijini hapa jana.
Kunambi alisema, kuwa Dodoma ipo katikati ya Tanzania bara ikiwa ni kitovu cha barabara kutoka Dar es Salaam ambapo kuna bahari ya Hindi inayounganisha nchi za maziwa makuu,na kwamba Dodoma ni eneo la kimkakati kwa Tanzania na nchi za maziwa makuu.
Alisema Dodoma inakuwa kituo muhimu kwa mizigo inayopitishwa kwa njia ya barabara na reli, na kwamba kutokana na umuhimu huo, halmashauri imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 507 kwa ajili ya uwekezaji wa bandari kavu na maghala huku lengo la uwekezaji huo ikiwa ni kuwarahisishia uchukuaji wa mizigo nchi za maziwa makuu badala ya kuifuata bandari ya Dar es Salaam.
Kongamano la uwekezaji ngazi ya Mkoa limefanyika kwa siku mbili katika Halmashauri ya jiji la Dodoma likihudhuriwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waliopata fursa ya kujadili fursa za uwekezaji na kutembelea maeneo mbalimbali yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na miradi mikubwa ya uwekezaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.