MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini.
Kwa mujibu wa EWURA, mwezi huu bei hizo zimeongezeka, ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Godfrey Chibulunje imebainisha kuwa bei hizo mpya, zitaanza kutumika kuanzia leo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa Septemba bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa, zimeongezeka kwa Sh 20 kwa lita (sawa na asilimia 1.11), Sh nane kwa lita (sawa na asilimia 0.46) na Sh 124 kwa lita (sawa na asilimia 7.93).
“Ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeongezeka kwa shilingi 20.19 kwa lita (sawa na asilimia 1.18), shilingi 8.14/lita (sawa na asilimia 0.49) na shilingi 123.89/lita (sawa na asilimia 8.58),”ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa jana.
Ilieleza kuwa mwezi huu bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimepungua ikilinganisha na bei zilizotolewa mwezi uliopita.
Taarifa ilieleza kuwa bei hizo zimepungua kwa petroli na dizeli kwa Sh 19 kwa lita (sawa na asilimia 1.04) na Sh tano kwa lita (sawa na asilimia 0.25), mtawalia.
Vilevile, ilieleza kuwa ukilinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimepungua kwa Sh 19.35 kwa lita (sawa na asilimia 1.11) na Sh 4.51 kwa lita (sawa na asilimia 0.27), mtawalia.
Taarifa ya Chibulunje ilieleza kuwa bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Agosti 5, mwaka huu.
“Hii ni kwa sababu, kwa mwezi Agosti hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa ilieleza kuwa, mwezi huu bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) zimeongezeka ikilinganisha na bei zilizotolewa mwezi uliopita.
Ilibainisha kuwa mwezi huu, bei hizo za rejareja za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa Sh 11 kwa lita (sawa na asilimia 0.60) na Sh 16 kwa lita (sawa na asilimia 0.91), mtawalia.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo vilevile, ukilinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa Sh 11.19 kwa lita (sawa na asilimia 0.64) na Sh 16.36/lita (sawa na asilimia 0.98).
Alisema mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani, yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za usafirishaji na gharama za ucheleweshaji wa ushushaji wa mafuta.
“Ewura inapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini,” ilieleza taarifa hiyo.
Ilieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petrol, zitaendelea kupangwa na soko.
“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta,”ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa ya Chibulunje ilisisitiza kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, ilimradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Namba 74 la Februari mwaka huu).
“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika,” ilielekeza taarifa hiyo.
Chanzo: HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.