Na; Francisca Mselemo
MKUTANO wa mwaka wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma umefanyika Leo Agosti 15,2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Jiji, ukiwa na ajenda muhimu za kujadili mipango iliyotekelezwa na matumizi yaliyofanyika katika mwaka wa fedha uliopita, yaani 2023/2024, pamoja na uchaguzi wa Naibu Meya, wenyeviti,na wajumbe wa kamati za kudumu za Halmashauri.
Katika mkutano huu, Madiwani walijadili masuala mbalimbali yanayohusiana na utendaji, ikiwa ni pamoja na huduma za Afya na ukusanyaji wa mapato. Moja ya matukio muhimu katika mkutano huo, ilikuwa ni uchaguzi wa Naibu Meya,huku Mgombea katika uchaguzi, akiwa mmoja tu ambaye ni mheshimiwa Fadhili Chibago,diwani wa kata ya Dodoma Makulu.
Kwa mujibu wa kanuni,Wajumbe walitakiwa kupiga kura za ndiyo au hapana,ndipo zoezi la kupiga kura lilipofanyika, kura zilizopigwa zilikuwa 47, kura moja iliharibika,kura 46 zilikuwa za ndiyo,hatimaye, baada ya mchakato wa uchaguzi, Naibu Meya mpya alipatikana, akitarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Madiwani na Menejimenti ya Jiji.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo yaliyompa ushindi,Naibu Meya huyo mpya alikuwa na haya ya kusema,
“ Nawashukuru sana kwa kunichagua kwa kura nyingi,nashukuru sana kwa heshima mliyonipa,na imani kubwa mliyoionyesha kwangu.Lakini Mimi bila ninyi,siwezi,nawategemea sana tushirikiane katika kila jambo,mnishauri,na mnionye pia pale nitakapokosea.Nawashukuru sana,na nawaahidi utumishi makini sana,utumishi bora”.
Aidha,mkutano huo pia ulijumuisha uchaguzi wa wajumbe na wenyeviti wa kamati za kudumu za Halmashauri. Kamati hizo zina jukumu muhimu la kusimamia shughuli mbalimbali za Halmashauri na kuhakikisha kwamba Wananchi wanapata huduma bora,na mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.Wajumbe walichaguliwa kwa kuzingatia ujuzi wao, uzoefu, na uwezo wa kushirikiana na Wananchi katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, mkuu wa idara ya Mipango na uratibu wa Jiji,ndugu Francis Kaunda aliwasilisha taarifa ya Kiutendaji ya mwaka iliyojumuisha,mapato na matumizi.
“Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya jiji la Dodoma ilipanga kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 123.8,ilifanikiwa kutumia bilioni 131.Sisi Halmashauri ya Jiji la Dodoma,tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi.Fedha ambazo hazikuwa kwenye bajeti ya Halmashauri,lakini zimesababisha utekelezaji wa miradi mikubwa’’.Alisema Kaunda.
Kwa ujumla, mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma ulikuwa na mafanikio, ukionyesha dhamira ya Madiwani katika kuboresha Huduma za Jamii na maendeleo ya Jiji. Hali hii inatoa matumaini makubwa kwa wananchi wa Dodoma wanaotarajia kuona mabadiliko chanya kupitia Uongozi mpya.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.