FAMILIA zimekumbushwa kujadili masuala ya maadili ili kujiepusha na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayotajwa kukithiri ndani ya jamii katika siku za hivi karibuni
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alitoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mayamaya, kata ya Zanka, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Familia hapo Mei 15, 2023.
Alibainisha kwamba kasi ya kuporomoka kwa maadili inachochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana wamekuwa wakiiga tamaduni na desturi za jamii zingine zinazokinzana na mila na desturi za mtanzania.
"Maadhimisho haya yanawakumbusha wazazi wote wawili na walezi wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto na familia hasa maeneo makuu matatu ya msingi ambayo ni kumjali mtoto kwa mahitaji ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na kufahamu maendeleo yake kwa ujumla" alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima ametaja changamoto za kiuchumi ndani ya familia kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ambapo wazazi au walezi wamejikuta wakitumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kusahau wajibu wao wa kusimamia malezi na makuzi yenye maadili mema kwa watoto.
"Mtoto anaanzishwa kufanyiwa vitendo vya ukatili toka mdogo hadi anakwenda kufundisha na wengine shuleni na mzazi upo, mbona Ng'ombe na mbuzi mnawafuatilia kuliko watoto, Maadili yanatengenezwa kwenye familia, nyumba za ibada, shuleni na vyuoni ili mtoto apite kote akutane na maadili hivyo tumieni muda wenu kuwafatilia watoto " alisema Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhimiza maadili mema na upendo ndani ya familia, bado kuna matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto katika familia, shuleni na kwenye jamii ikiwemo ukatili mitandaoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.