Na. Mwandishi Maalum, DODOMA
TIMU ya wasichana ya mpira wa miguu ya Fountain gate imepongezwa kwa kuibuka bingwa wa mashindano ya shule za sekondari za Academy yaliyoandaliwa na CAF Africa ukanda wa CECAFA na kuichora ramani ya Jiji la Dodoma kwenye mpira.
Pongezi hizo zilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika hafla kabambe ya kuipokea na kuipongeza timu ya wasichana ya mpira wa miguu ya Fountain gate katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa timu hiyo ya wasichana imeichora ramani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenye mpira. “Hakuna Mstahiki Meya yeyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakati huu anayeongea na mabibwa wa CECAFA isipokuwa Meya wa Jiji la Dodoma. Hivyo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma tumekuwa kinara kwenye mambo mengi sana, lakini mabinti hawa wa Fountain gate mmetung’arisha zaidi” alisema Prof. Mwamfupe.
Aidha, Mstahiki Meya huyo alishauri kuwa liandaliwe bango kubwa la chuma lenye majina na picha za wasichana hao mabingwa wa CECAFA katika shule ya sekondari ya Fountain gate ili iwe kumbukumbu kwao na vizazi vijavyo.
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa wanafunzi wa kike wa shule ya sekondari Fountain gate wameipa heshima Halmashauri ya Jiji la Dodoma na taifa kwa ujumla. “Mabinti wa Fountain gate wameleta heshima kwa Mkoa wa Dodoma, wameleta heshima kwa Jiji la Dodoma, wameleta heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua ubingwa wa CECAFA” alisema Rweyemamu.
Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji inajivunia mabinti hao kwa kudhihirisha umuhimu wa michezo kwa wanafunzi. “Mheshimiwa mgeni rasmi, mabinti hawa wanafanya vizuri katika taaluma. Hakika wamedhihirisha kuwa taaluma na michezo vinakwenda pamoja. Hapa tunazungumza na mabinti wanaokwenda Afrika ya Kusini kutetea ubingwa wa CECAFA” alisema Mwalimu Rweyemamu wakati akitabasamu.
Aidha, aliwataarifu kuwa michezo ni ajira. Kupitia michezo alisema kuwa wamekuza uchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
Mashindano ya CECAFA kwa shule za sekondari yalianza tarehe 16-19 Februari, 2023 jijini Dar es Salaam na timu ya wasichana ya Fountain gate ya jijini Dodoma iliibuka kidedea ikiwa na wachezaji 15 na walimu wa nane ilitunukiwa dola za kimarekani 100,000.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.