WAKAZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufuata sheria zilizopo kabla ya kuanza ujenzi ili kuepuka kujenga kinyume na taratibu za mipango miji nchini na kulifanya Jiji hilo kujengeka kiholela.
Rai hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu namba moja ya wajumbe wa menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alipokuwa akiongelea utekelezaji wa zoezi hiko lililoanza mapema asubuhi jijini hapo leo.
Kimaro ambaye pia ni mkuu wa idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu alisema kuwa kumekuwepo na tabia inayoendelea kukua ya kujenga bila kuwa na vibali vya ujenzi. “Tumefanya ziara ya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ambayo ujenzi unaendelea. Hii ni baada ya Halmashauri ya Jiji kubaini watu wengi wanafanya uendelezaji na ujenzi ambao hauna vibali na kutozingatia taratibu za uendelezaji wa mji. Tulichobaini katika timu yetu, watu wengi wanafanya ujenzi bila kuwa na vibali vya ujenzi. Na kwa kweli tumewasimamisha wasiendelee na ujenzi mpaka watakapopata vibali halali vya ujenzi” alisema Kimaro.
“Katika ukaguzi huu tumebaini mambo ya ajabu sana. Unakuta maeneo ya makazi yaliyopimwa lakini kuna biashara ambazo zimeanzishwa za kufyatua tofali kinyume ya masharti ya kibali na matumizi ya eneo husika” alisema Kimaro.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Dodoma, kuhakikisha kabla ya kuanza ujenzi wanafuata taratibu zote za mipango miji ambazo ni kuwa na ramani zilizopitishwa na mamlaka husika, kuwa na vibali sahihi vya ujenzi ambavyo vimepitishwa na mamlaka na Jiji, na kujiepusha na ujenzi holela usiofuata taratibu. “Kukiuta kufuata utaratibu kutasabisha kuvunjiwa majengo hayo. Wananchi wote wanatakiwa kutii sheria bila shuruti” alisisitiza Kimaro.
Kwa upande wa fundi sanifu ujenzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Issac Emmanuel alisema kuwa changamoto kuwa ni maeneo yaliyopimwa watu wanajenga tofauti ya masharti ya vibali vyao vya ujenzi.
“Yapo maeneo ambayo yamepimwa, unakuta mtu kapewa kibali cha ujenzi wa nyumba moja ila anajenga ‘two in one’. Maeneo mbayo yamepangwa kwa makazi tu, unakuta mtu kajenga fremu za biashara. Maeneo yametengwa kwa ajili ya makazi, mtu anajenga taasisi bila kuwa na kibali chochote. Unakuta watu wengine wanaendelea na ujenzi wakati vibali vyao havijapitishwa na Halmashauri” alisema Emmanuel kwa masikitiko.
Timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilijigawa katika makundi manne, na kundi hili kutembelea maeneo ya Itega, Kinyambwa na Kikuyu kukagua ujenzi usiozingatia taratibu.
Mwenyekiti wa Kundi Na. 1 la Timu ya Menejimenti ya Jiji la Dodoma Dickson Kimaro (kulia) akiwa na maafisa wengine wa Jiji la Dodoma Omari Mafia (kushoto) na Isaya Kimei (kushoto kwa Mafita) wakikagua vibali vya ujenzi kutoka kwa msimamizi wa ujenzi wa moja ya maeneo waliyotembelea kubaini wanaojenga bila kufuata taratibu halali za ujenzi.
Baadhi ya maeneo yaliyokutwa ujenzi ukiendelea bila kufuata taratibu za ujenzi na kuzuiliwa kuendelea na ujenzi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.