MRADI wa ujenzi wa Government City Complex utaiwezesha Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujitegemea kimapato baada ya kukamilika kwake.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akimshukuru Kiongozi wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 baada ya kuweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Government City Complex jijini Dodoma.
Shekimweri alisema “mradi huu utatufanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuweza kujitegemea kimapato”. Sifa ya halmashauri yenye hadhi ya jiji ni uwezo wa kujitegea kimapato, aliongeza na kuutaja mradi huo kuwa umetafsiri maana ya serikali kuhamia Dodoma.
Akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi mradi huo, Kiongozi wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Lt. Josephine Mwambashi aliwataka wanaosimamia miradi ya serikali kuwa makini. “Lazima tuwe makini kusimamia miradi hii, ioneshe kuwa tupo na uzalendo usio na shaka. Niwatake kuzidisha ushirikiano kwenye utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo” alisisitiza Lt. Mwambashi.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Government City Complex kwa Kiongozi wa mbio hizo, Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shaban Juma alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza mapato ya halmashauri na kutoa huduma kwa wananchi.
Akiongelea ujenzi wa mrahi huo, alisema kuwa utekelezaji wake ulianza tarehe 1 Septemba, 2019 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 31 Disemba, 2020. “Hata hivyo mkandarasi aliongezewa muda hadi tarehe 31 Agosti, 2021. Mradi huu unatekelezwa na mkandarasi M/S Mohammed Builders Ltd. Chanzo cha fedha za mradi huu ni mapato ya ndani” alisema Juma.
Kuhusu matumizi ya TEHAMA, mkuu huyo wa idara alisema “majengo yatatumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA kama vile mfumo wa ukusanyaji wa mapato, mfumo wa ulinzi kwa kutumia camera, mfumo wa ving’amuzi moto, mfumo wa kununua vyumba kwa mtandao na uwepo wa huduma za mtandao za bure.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.