WADAU wametakiwa kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye kuhakikisha jamii inabadili fikra kuhusu lishe na kuona umuhimu wa Lishe Bora kwa Ustawi wa Taifa.
Akizungumza na wananchi pamoja na Wadau wa Lishe wakati wa Mkutano Mkuu wa 8 wa Lishe uliofanyika Mkoani Mara, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema atafuatilia ufanisi wa wadau kwenye kuwatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii kwani ndiyo wenye taaluma ya kubadilisha fikra za jamii.
"Maafisa Maendeleo ya Jamii ni wataalam wa kubadilisha fikra za Jamii, wakati wataalam wa Lishe ni wanatumia taaluma yao kutengeneza mikakati ya lishe ili ikubalike kwenye jamii hivyo katika eneo hili tupo pamoja tutashirikiana" amesema Waziri Gwajima.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuungana ili kupata matokeo mazuri ya utekelezaji wa afua za lishe ikiwemo kushirikiana Jamii yenyewe pamoja na sekta nyinginezo ikiwemo viongozi wa Dini na Mila.
Waziri Dkt. Gwajima pia amewakumbusha walimu na Wazazi kuacha kuwaadhibu watoto kwa kiwango kikubwa pale wanapoona hawaelewi, amesema wakati mwingine inatokana na lishe duni inayoathiri afya ya akili, hivyo wawashirikishe na wataalam wa Lishe kutatua changamoto hiyo.
Aidha, amevitaka vikundi vyote vya Jamii vinavyojitolea, ikiwemo SMAUJATA, Skauti, Girl Guides, Redcross, Mabaraza ya Wazee, Majukwaa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Mabaraza ya Watoto na jumuiya za kivyama kubeba Ajenda za kimkakati za maendeleo ya jamii ikiwemo Ajenda ya Lishe ili kuhakikisha Ajenda hiyo inaifikia jamii.
"Kwa sababu Wizara yangu ndio lango la kuingia kwenye jamii, Taasisi ya lishe tukae pamoja kupitia Wizara mama tuone tunawezeshaje vikundi hivi ili kujua wamefikia jamii Kwa kiasi gani" amesisitiza Dkt. Gwajima
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.