WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati nchini na kwamba hakuna mradi wowote utakaokwama.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo Jumapili, Oktoba 16, 2022 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Daraja la Magufuli (Kigongo - Busisi) ambao umefikia asilimia 53.66 na Reli ya Kisasa (SGR) wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
"Wale wenye mashaka kuhusu miradi hii, niwahakikishie hakuna mradi utakaokwama, miradi yote iliyoanzishwa na Serikali yeru ya Chama Cha Mapinduzi itakuwa endelevu na itakamilika, miradi hii yote inalenga kuwanufaisha Watanzania na Rais Samia anaiendeleza miradi yote."
Waziri Mkuu ameongeza kuwa ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati, Serikali imeendelea kuhakikisha hakuna mkandarasi yeyote atakayecheleweshewa malipo pindi anapotoa hati ya madai.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakazi wa wanaoishi maeneo yanayozunguka maeneo miradi hiyo watumie fursa hiyo kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za kulala wageni.
Vile vile, Mhe. Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha anaimarisha ulinzi katika maeneo yote yanayotekelezwa miradi hii ili kuzuia vitendo vya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo saruji na nondo.
Aliongeza kuwa Watanzania waliopata ajira kwenye miradi hiyo wahakikishe wanakuwa mahiri kwenye maeneo wanayofanyia kazi. "Kama wewe unakunja nondo hakikisha unakuwa mahiri kwenye eneo hilo, kama wewe unaendesha mitambo hakikisha unakuwa mahiri, tunataka muwe mafundi mahiri kwenye kila eneo ili tunapoanza miradi mingine tuwe na wataalam wa kutosha."
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.