WITO umetolewa wa Maafisa usafirishaji wa Bajaji na Pikipiki (Bodaboda) Jijini Dodoma kufuata sheria za barabarani zilizowekwa na Mamlaka husika ili kuepuka kadhia wanazozipata pindi wanapokua kazini. Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokutana na kundi hilo kwenye ukumbi wa ofisi yake iliyopo jengo la Mkapa.
Mkuu wa Mkoa huyo, ameitisha kikao hicho ikiwa ni utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii yaliyopo ndani ya Mkoa wa Dodoma kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili. Katika kikao hicho, kero kadhaa ziliwasilishwa na nyingi zikapatiwa ufumbuzi ikiwemo ya uvunjaji wa sheria za barabarani ambapo amewataka madereva hao kufuata sheria kwa ustawi wa Mkoa.
“Sheria hizi zimewekwa ili tuzifuate na hakuna sheria iliyowekwa kwa ajili ya kumkandamiza mwananchi. Lengo hasa ni kuimarisha ulinzi na usalama wa raia. Nyinyi ni viongozi, kaeni na wenzenu munapokua kwenye vituo vyenu, peaneni ushauri wa namna ya kujiendeleza kwenye mambo ya msingi.
“Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini makundi yote ya kijamii yaliyopo katika maeneo yetu na yote anayapa uzito ulio sawa hivyo na sisi tunapaswa kufanya hivyo kwani Rais wetu anatamani kila mmoja awe na furaha.” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Akijibu Baadhi ya kero zilizowasilishwa kwenye kikao hicho ambazo nyingi zililenga Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini LATRA inayojishughulisha na utoaji wa leseni za usafirishaji, Ezekiel Emmanuel ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo amesisitiza umuhimu wa kuwa na leseni ya usafirishaji ili kuepuka kadhia barabarani
“Mtu yeyote anayekusudia kufanya shughuli ya usafirishaji wa abiria, sharti nawe na leseni ya LATRA. Kinyume na hapo ni kosa la jinai na atapigwa faini ya shilingi 25,000. Tutii sheria bila shuruti kuepuka ukamataji holela. Tuhamasishane kwenye vituo vyetu kuepukana na haya. Tunatafuta riziki lakini sio kwa uvunjifu wa amani” Amesema Emmanuel.
Jiji la Dodoma lina takribani vituo vya Bajaji na Bodaboda 394 vilivyosajiliwa huku waendesha vyombo hivyo waliosajiliwa wakifikia takribani 400. Mkoa unathamini mchango wa sekta ya usafirishaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.