MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amewataka wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika vituo vya uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Kauli hiyo aliitoa muda mfupi baada ya kujiandikisha katika kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Nyerere, kilichopo Mtaa wa Nyerere, Kata ya Kilimani leo asubuhi.
Dkt. Mahenge alisema kuwa zoezi la uandikishaji linaenda vizuri. Alisema kwa siku tatu za kwanza za uandikishaji huo, jumla ya wananchi 393,534 walijiandikisha, sawa na asilimia 38.23. Alisema kuwa maoteo ya uandikishaji ngazi ya mkoa ni kuandikisha wananchi 1,029,265. “Jana mvua ilinyesha maeneo mengi na baadhi ya watu kushindwa kujitokeza kujiandikisha. Nataka nitumie fursa hii kwamba leo hali ya hewa ni nzuri wananchi waende kujiandikisha kwa wingi” alisema Dkt Mahenge. Tukiongeza juhudi, tutafikia lengo la uandikishaji, aliongeza.
Kwa upande wake, Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa hali ya uandikishaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea vizuri. Katika siku tatu za uandikishaji kuanzia tarehe 8 - 10 Oktoba, 2019, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeandikisha wananchi 45,717, kati yao wanaume ni 23,987 na wanawake ni 21,730 alisema.
Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 utafanyika tarehe 24 Novemba, 2019 ukiongozwa na kaulimbiu isemayo “Viongozi bora wa Serikali za Mitaa ni chachu ya maendeleo, ni haki na wajibu wako kujiandikisha, kugombea na kuchagua kiongozi bora”.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akipata maelekezo kutoka kwa Afisa Mwandikishaji wa Kituo cha kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2019 nchini kote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.