HALMASHAURI 55 nchini zimenufaika na awamu ya kwanza ya mgao wa fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi nchini.
Mkataba wa kutekeleza mradi huo umesainiwa baina ya Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Halmashauri zinazotekeleza mradi huo ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu amezielekeza halmashauri hizo kuhakikisha kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo kiwe ni kupanga miji midogo inayochipukia.
"Ili miji inayochipukia iweze kukua katika utaratibu mzuri ni lazima ipangwe, ipimwe na watu waweze kumilikishwa ardhi huku maeneo ya huduma za kijamii yakiwekwa wazi ili hata baadaye wakati wa uendelezaji watu wasipate shida ya kutafuta maeneo ya huduma."
Aidha, Mhe. Ummy amewapongeza viongozi wa Wizara ya Ardhi kwa maono ambayo yatasaidia katika kupanga miji na kuongeza mapato ya halmashauri.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema halmashauri zilizopata fedha hizo zikatumie kwa kazi iliyokusudiwa ili watakaporejesha na halmashauri zingine ziweze kunufaika.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amesema kati ya halmashauri 78 zilioomba mradi huu, zilizokidhi vigezo vya kupata fedha ni 55 tu katika awamu hii ya kwanza.
“Fedha hizi za mikopo zinatolewa kwa halmashauri zilizokidhi vigezo ikiwemo uwasilishaji wa maandiko ya miradi ya upangaji na umilikishaji ardhi ikionesha utayari wa kufanya kazi hizo kwa kuwamilikisha wananchi maeneo yao na pia kuiwezesha Serikali kukusanya mapato” amesema Mhe. Lukuvi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.