MAMLAKA za Serikali za Mitaa nchini zimetakiwa kujipima na kujitathmini katika ukusanyaji wa mapato kwa mujibu wa malengo ya ukusanyaji kodi.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa 35 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli jijini Mwanza jana.
Majaliwa alisema Halmashauri zinatakiwa kujitathmini juu ya ukusanyaji wa mapato yao ya ndani kulingana na malengo waliyojiwekea.
“Kuna Halmashauri zimetajwa hapa kwamba hazijafikia malengo ya makusanyo ya ndani. Fanyeni tathmini, ni kwa nini hamjafikia malengo na mhakikishe kuwa mwakani hamji kutajwa tena kwenye mkutano kama huu”, alisema Majaliwa. Halmashauri hizo ni Kakonko, Buhigwe, Madaba, Kigoma, Momba na Songea.
Waziri mkuu aliwataka Meya, Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Mamkala za Serikali za mitaa kusimamia makusanyo na matumizi ya mapato ili yatumike katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini. Aidha, aliwataka kutenga asilimia 40 kwa ajili ya shughuli za maendeleo kutoka kwenye makusanyo ya ndani. Alisema kuwa dhamira ya serikali ni kuona Halmashauri zinajitegemea kwa asilimia 80-100 ifikapo mwaka 2025.
Akiongelea uamuzi wa serikali kukusanya fedha zote na kuziweka katika chanzo kimoja, alisema kuwa uamuzi huo ulitokana na utafiti wa muda mrefu uliobaini kuwa fedha zilizokuwa zinakusanywa zilikuwa haziendi kwenye miradi ya maendeleo inayowalenga moja kwa moja wananchi.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, Mhe. Selemani Jafo (Mb) alisema kuwa serikali inajivunia ujenzi wa shule za sekondari za Kata. Alisema kuwa shule hizo zimefanya vizuri katika mtihani wa kumaliza kidato cha sita mwaka 2019. “Kati ya shule bora 100, shule 64 ni za Serikali na kazi ya shule hizo 64, shule 54 ni za kata. Na kwenye matokeo ya masomo ya sanaa, kati wanafuzi bora 10 wa kiume, wanafunzi saba wanatoka kwenye shule za kata,” alisema Jafo.
Waziri huyo aliipongeza Serikali kwa kutenga sh. bilioni 268.8 kwa ajili ya ujenzi wa miradi 38 ya kimkakati kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo ni ujenzi wa stendi za mabasi, masoko na machinjio.
Mkutano wa ALAT unafanyika jijini Mwanza kwa siku tatu ukihudhuriwa na washiriki zaidi ya 600 wakiwemo Mameya wa Majiji na Manispaa, Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za mitaa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifurahia jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), katika mkutano mkuu wa 35 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), uliyofanyika katika ukumbi wa Malaika, jijini Mwanza, Waziri Mkuu amemwakimwakilisha Rais Magufuli katika mkutano huo, Julai 23.2019.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.