Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma itapitia taarifa za kila kata, kuzichambua na kubaini changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kuzitatua ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru katika Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kuwasilisha taarifa za utekelezaji za robo ya tatu (Januari-Machi, 2023) kutoka kwenye kata uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mafuru alisema “leo tumefanya kikao kifupi lakini cha kisanyansi. Taarifa hizi kutoka kwenye kata tutazichambua na kubaini changamoto za kiutendaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzitatua. Lengo ni kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi”.
Alisema kuwa halmashauri imeandaa makala za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata za halmashauri hiyo na itakuwa ikioneshwa katika vikao vya robo. Alisema kuwa makala hizo ni muhimu kwa madiwani wa halmashauri hiyo kuwa na picha halisi na uelewa wa pamoja wa miradi inayotekelezwa kwenye kata.
Kwa upande wake Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa halmashauri inatekeleza miradi mingi ya maendeleo kupitia mapato ya ndani, serikali kuu wa wahisani mbalimbali. “Kila robo tutakuwa tunaonesha makala ya miradi yote iliyotekelezwa katika kata. Makala hiyo itaonesha jina la mradi, hali ya utekelezaji na kiasi cha fedha kilichopelekwa kwa kila kata ili kuweka uwazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo” alisema Kaunda.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.