Na. Josephina Kayugwa, DODOMA.
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma yatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutaka halmashauri zote zijisimamie kimapato, kwa kujenga miradi mbalimbali ya kimkakati kupitia fedha za ndani itakayoiongezea halmashauri hiyo mapato.
Akiongea katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Jiji la Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa Madiwani kutoka Zanzibar waliofika kwaajili ya kujifunza na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kujenga miradi ya kimkakati kama Soko la wazi la Machinga, Jengo la kitega uchumi Mtumba, Maegesho ya malori Nala na Hoteli ya nyota nne Dodoma City Hotel.
“Mapato ya ndani yameifanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ifanikishe kujenga miradi mbalimbali ambayo itaongeza mapato kwenye Halmashauri, haya yote yamefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri baina ya Madiwani na wataalamu waliopo ndani ya Halmashauri,”
“Kupitia miradi hii tunaona jinsi gani Jiji la Dodoma limejipanga kujisimamia kimapato kwa zaidi ya asilimia 100 na kutekeleza maagizo yote ya kimkakati,” aliongezea Kaunda.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kikwajuni Zanzibar, Ibrahim Fataki alisema katika ziara hii amejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi ambavyo Jiji la Dodoma limeweza kujisimamia kimapato na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kupitia mapato ya ndani.
“Mimi nimejifunza mengi nimeona namna gani wanaendeleza mipango miji pia nimethibitisha kuwa Jiji la Dodoma lina utanuzi mkubwa na mafanikio makubwa katika Serikali ya Tanzania, tukitoka hapa tunakwenda kuona jinsi gani na sisi mipango yetu tutakavyoipanga katika miji yetu,” alisema Fataki
Sambamba na hilo aliishukuru Halmashauri ya Jiji kwa mapokezi mazuri na kutoa ushauri kwa Halmashauri nyingine za Tanzania bara na Zanzibar, kutembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwaajili ya kujifunza mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.