Na. John Masanja, DODOMA
“Sisi kama Waheshimiwa Madiwani tupo tayari kusaidiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kutoa taarifa juu ya watu wanaoficha sukari, lakini tuendelee kuviamini vyombo hivi kwa juhudi zinazofanyika juu ya changamoto hii”
Hayo yalisemwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe katika Mkutano wa Baraza la Madiwani Robo ya pili (Oktoba – Desemba) 2023/2024 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aidha, Prof. Mwamfupe alisisitiza ushirikishwaji wa viongozi ngazi ya kata na mitaa katika uendeshwaji wa oparesheni hiyo kwa sababu imekuwa ni changamoto katika jamii. Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakificha sukari hali inayofanya bei yake kupanda na kuadimika katika soko.
Awali akifungua mkutano huo, Prof. Mwamfupe alitoa taarifa ya kuanzishwa kwa mfumo wa ufundishaji mubashara (E- Learning) wa kujifunzia kupitia Tehama katika Shule ya Sekondari Dodoma ikiwa ni mmoja kati ya shule 10 nchini zilizochaguliwa kwa majaribio ya awali.
Kufuatia umuhimu wa mfumo wa ufundishaji mubashara, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI- Mohamed Mchengerwa aliziagiza halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya uanzishaji wa mfumo huo hadi kufikia mwaka 2025.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo aliahidi kulifanyia kazi suala la ujenzi holela wa vizimba pembezoni mwa Soko la wazi la Machinga wakati akijibu swali la papo kwa papo lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Majengo, Shifaa Ibrahim aliyetaka kufahamu Jiji limejipanga vipi kushughulikia suala la ujenzi holela wa vizimba pembezoni mwa soko hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.