Na Sifa Stanley, DODOMA.
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe amesema kuwa halmashauri hiyo inatarajia kuwa na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia hamsini kwa kipindi kifupi kijacho, ambapo kwa sasa ina uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 42.
Alisema hayo wakati wa mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kupitia taarifa ya ufungaji hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2020/2021 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Mipango Jijini Dodoma.
Mstahiki Meya Prof. Mwamfupe alisema kuwa juhudi za Mkurugenzi na Madiwani zimesaidia mapato ya halmashauri kuongezeka na kuifanya halmashauri kuwa na uwezo wa kujitegema kwa asilimia 42 hadi kufikia mwezi Juni 2021.
“Hongera sana Mkurugenzi na timu yako mmeweza kukamilisha kwa wakati taarifa ya hesabu, na kinachofurahisha zaidi ni uwezo wa kujitegemea, kama tumeweza kujitegemea kwa asilimia 42 tumebakiza asilimia 8 tungeweza kujitegemea kwa muda wa miezi sita, tulianza na asilimia 34 lakini sasa hivi tunakwenda vizuri, hongereni sana madiwani kwa matumizi mazuri na ukusanyaji mzuri wa mapato” alisema Prof. Mwamfupe.
Awali akiwasilisha taarifa hiyo ya hesabu mbele ya wajumbe wa baraza hilo, Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA Rahab Philip alisema kuwa, uwezo wa kujitegemea umeongezeka kutoka asilimia 34 mwaka juzi hadi asilimia 42 mwaka jana hali inayoonesha kuwa tunapiga hatua.
“Mheshimiwa mwenyekiti, uwezo wa kulipa madeni unapimwa kwa kulinganisha mali za muda mfupi yaani ndani ya mwaka mmoja na madeni yanayotakiwa kulipwa ndani ya mwaka huo. Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za fedha, uwiano wa 2:1 yaani thamani ya mali za muda mfupi inatakiwa kuwa mara mbili ya madeni ya muda mfupi. Uwezo wakulipa madeni kwa 2020/2021 umepungua kutoka uwiano wa 3.1:1 ya mwaka uliopita hadi 1.5:1 mwaka huu" alisema CPA Rahabu.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Mwamfupe, kilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ambaye ndiye Katibu, wajumbe ambao ni madiwani, wakuu wa idara pamoja na wageni mbalimbali.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akiongea wakati wa Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani uliohusu Taarifa ya Ufungaji Hesabu za Halmashauri ya Dodoma kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA Rahab Philip alipokuwa akijibu hoja na kutolea ufafanuzi vipengele vya taarifa iliyowasilisha mbele ya Baraza la Madiwani.
Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Awadh Abdallah akichangia wakati wa Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dodoma.
Diwani wa Kata ya Chang'ombe, Mhe. Bakari Fundikila alichangia hoja mara baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Ufungaji wa Hesabu za Halmashauri kwa mwaka wa Fedha 2020/2021.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.