HALMASHAURI za Mkoa wa Dodoma zimetakiwa kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga shilingi Bilioni 7.5 katika mapato yake ya ndani kujenga jengo la kisasa la Machinga ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri.
Ushauri huo ulitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi jengo la kisasa Machinga katika eneo la Bahi road jijini Dodoma iliyofanyika siku ya Alhamisi tarehe 13 Januari, 2022..
Dkt. Mganga alisema “nichukue fursa hii kusema neno moja, mradi huu ni mkubwa wa shilingi bilioni saba pointi. Hiyo bilioni saba haijatoka serikali kuu, lazima tulifahamu hili. Hii bilioni saba ni mapato ya ndani ya Jiji la Dodoma. Tunaposema kutumia asilimia 40 kuleta maendeleo hii ndilo tunalolieleza. Kwamba tunasubiri kwamba kila mradi mkubwa fedha zitoke serikali kuu, lakini katika hili iwe mfano, kama hii Machinga complex inajengwa kwa mapato ya ndani ya Jiji hii ndiyo ile kauli ya viongozi wetu wanavyosema fedha tunazokusanya kwenye mapato ya ndani ya halmashauri zitumike kuleta maendeleo katika halmashauri. Katika hili, Jiji wanapaswa kupongezwa sana. Hili ni funzo, halmashauri zetu nyingine za Mkoa wa Dodoma ziige mfano huu. Tuwe na miradi ya asilimia 40 yenye tija ambayo inaonekana kabisa hizo fedha thamani yake inaonekana na inakwenda kutatua changamoto za wananchi moja kwa moja. Katika hili Jiji niwapongeze sana”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa eneo hilo linalojengwa lina uwezo wa kuweka Machinga 3,000 na kuongeza kuwa eneo hilo linauwezo wa kuongeza Machinga hadi kufikia 5,000. “Kama tulivyokubaliana kwenye kikao cha ndani tunaendelea kusajili Machinga wote kwa njia ya kieletroniki ili wale tulioanza nao 3,000 wa kwanza wawe wa mwanzo kuingia katika mradi huu” Sisi kama Jiji ambacho tunaweza kukuhakikishia Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa fedha tunayo tumetenga kwenye bajeti. Tutamsimamia Mkandarasi ili akamilishe kama tulivyokubaliana kufikia tarehe 17 Machi, 2022 atukabidhi mradi ili uanze kutumika” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Aidha, alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa halmashauri itasimamia ili anayefanya kazi eneo hilo awe ni mtu anayestahili. “Hii mambo ya kujipachika ndiyo maana tunakwenda kwenye mfumo wa kietroniki. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mpaka sasa toka tuanze hatujapata changamoto yoyote tupo kwenye muda. Mkandarasi tumeshamlipa shilingi Milioni 841 kwa ajili ya kuendelea na mradi huu. Tunaimani mradi huu ukikamilika Dodoma itakuwa safi” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alifanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la Machinga akiambatana na Katibu Tawala Mkoa, Kamati ya Usalama ya Mkoa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi na maafisa waandamizi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.