Na; Happiness E. Chindiye
Habari - Dodoma RS
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, ametamatisha ziara yake ya kujitambulisha katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kufuatia uteuzi wake na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ziara hiyo ilianza Septemba 15, 2025 katika Halmashauri ya Mpwapwa na leo Septemba 18, 2025 imemalizika katika Halmashauri za Chamwino na Dodoma.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kazungu amewaelekeza Wakurugenzi Watendaji kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, hatua itakayosaidia kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuchochea maendeleo ya wananchi.
“Ni muhimu kila Halmashauri ikatenga maeneo ya kimkakati kwa ajili ya uwekezaji. Hatua hii itarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na pia kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wetu,” Amesema Dkt. Kazungu.
Aidha, Amewaelekeza Wakurugenzi watendaji kuandaa mikakati mipya ya kubuni vyanzo vya mapato ili kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchumi wa Mkoa wa Dodoma.
“Tusiishie kwenye vyanzo vya mapato vya jadi pekee. Ni lazima tuwe wabunifu, tuandike na kutekeleza mikakati mipya ya kuongeza mapato ili Dodoma izidi kusonga mbele kiuchumi,” Ameongeza.
Sambamba na hilo, Dkt. Kazungu amewahimiza watumishi wa serikali pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.