MAMLAKA za serikali za mitaa nchini zimeagizwa kujifunza kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma juu ya utekelezaji wa kanuni na sheria inayozielekeza mamlaka hizo kutenga asilimia 10 kutoka katika mapato ya ndani na kuwakopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Selemani Jafo muda mfupi kabla ya kukabidhi hundi ya shilingi 1,062,500,000 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika uwanja wa Nyerere square jijini hapa leo. "Naagiza Halmashauri zote ziige hiki kilichofanywa na Jiji la Dodoma" amekazia Waziri Jafo huku akiitaka Halmashauri ya jiji kufikiria miradi mikubwa zaidi itakayowaunganisha vijana wengi ili kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi na kuwafanya watu kutoka mataifa mengine kuja kujifunza Dodoma.
Jafo amesema “Leo tunakutana kwa jambo kubwa sana. Halmashauri ya jiji la Dodoma, ni Halmashauri ya mfano katika kuwezesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kutelekeza agizo la kuchangia asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa makundi hayo. Sababu kubwa ni uongozi bora na usimamizi makini wa rasilimali zinazokusanywa. Wana Dodoma sasa muone umuhimu wa kulipa kodi na tozo mbalimbali ili waendelee kukusanya na kurudisha kwenu”.
Vile vile, Waziri Jafo amewapongeza wanawake kwa wepesi na uaminifu wao katika kurejesha mikopo kila wanapokopa. “Pongezi kwa kina mama kwa sifa ya kurejesha mikopo. Mnaporejesha mikopo yenu, wengine wanapata fursa ya kukopa na kujiletea maendeleo. Hivyo, wito wangu kwenu muendelee kurejesha mikopo mnayokopa na mikopo hiyo ifanye kazi zilizokusudiwa” alisema Jafo.
Zaidi ya hayo, Waziri Jafo amewasifu maafisa maendeleo ya jamii wanavyofanya kazi kwa juhudi kubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo. Amesema, zamani maafisa maendeleo walikuwa wakitumika kama 'spare tyre' yaani kwenye baadhi ya matukio kama watu wa ziada. Lakini leo tunaona jinsi ambavyo wigo wa ukekelezaji wa majukumu yao umeongezeka na faida inaonekana. "Hongereni sana maafisa maafisa maendeleo ya jamii", alisema.
"Mwanzoni mwa mwaka 2018 nilikuwa na kilio kikubwa nikitamani mikopo hii inayotolewa isiwe na riba. Namshukuru sana Mungu ombi langu lilikubaliwa na rais wetu Mheshimiwa Magufuli na sheria ikapitishwa na tukaandaa kanuni zake na kuzipitisha pia, zikatoka kwenye gazeti la serikali na leo historia inawekwa katika kutekeleza ilani ya uchaguzi". Amesema Waziri Jafo kwa furaha.
Awali akiwasilisha taarifa ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka 2018/ 2019, Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa fedha za vikundi zinazokabidhiwa ni shilingi 1,062,500,000. Fedha hizo zinaifanya Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2019/2019 kutoa mikopo ya jumla ya shilingi 2,859,230,000 sawa na asilimia 109.6.
Akiongelea mchanganuo wa fedha hizo kwa vikundi, Kunambi alisema vikundi vya wanawake vinavyopatiwa mikopo ni 125, vinakavyopatiwa jumla ya shilingi 626,000,000. Vikundi vya vijana vipo 73, vitakavyopatiwa shilingi 419,000,000 na vikundi vya watu wenye ulemavu vipo 3, vinakavyopatiwa shilingi 17,500,000.
Katika salamu zake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa jiji lake linahakikisha kuwa vijana wanaopewa mikopo wanapewa na elimu ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na vyuo vya ufundi pamoja na chuo kikuu cha kilimo Sokoine. Lengo la kuwaunganisha na vyuo hivyo ni kuwawezesha kupata ujuzi ili uwasaidie kufanya kazi kwa weledi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.