Yaliyojiri Bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu tarehe 04/09/2019
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula.
Mkataba wa huduma kwa mteja (Client Service Charter) ambao unaweka bayana kuwa ndani ya siku thelathini (30) tangu nyaraka zifikishwe Ofisi ya Kanda kutoka Halmashauri, hatimiliki husika inapaswa kuwa imekamilika kwa hatimiliki za kawaida.
Kwa hatimiliki zitolewazo kwa njia ya mfumo unganishi wa kielektroniki (ILMIS) ulioanza kufanya kazi katika Wilaya za Kinondoni na Ubungo, hatimiliki inapaswa kuwa imekamilika ndani ya siku saba (7) tu.
Natoa rai kwa watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha kuwa wanakamilisha taratibu zote za umilikishaji kwa wakati.
Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa wizara itaendelea kuboresha taratibu za utoaji wa huduma hii muhimu ikiwemo kupunguza muda wa upatikanaji wa hatimiliki na kuwasogezea huduma katika ngazi za mikoa.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Mwaka 2008 Serikali kwa kushirikiana na UNICEF ilifanya utafiti kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto, utafiti huo unaonyesha kuwa asilimia 60 ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hufanyika nyumbani.
Vitendo hivi hufanywa na watu wa karibu na watoto wakiwemo baadhi ya wazazi, walezi, watoa huduma wa vyombo vya usafiri, majirani na wanafamilia.
Asilimia 40 ya vitendo vya ukatili hufanyika shuleni.
Sababu kubwa ya vyanzo vya ukatili ni imani potofu, elimu au hali duni ya umaskini, kutetereka kwa misingi ya malezi ndani ya familia, mila na desturi potofu na utandawazi.
Hakuna utafiti uliofanyika kuhusu ubakaji wa vikongwe, ingawa vyanzo vya ukatili vinashabihana na ule wa watoto.
Serikali itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutambua jukumu lao la malezi na matunzo kwa watoto na wazee (vikongwe) ambao ni hazina na tunu muhimu ya Taifa letu.
Chanzo: Idara ya Habari - MAELEZO.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.