Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa, haina upungufu wa chanjo wa aina yoyote hivyo kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto wao kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.
Dkt. Subi amesema kuwa, upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwa hiyo huitaji usafiri wa anga.
"Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo, chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa mikoa kumi na tatu ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD)".
Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikua wanazikosa, umeshaanza na watazipata kuwa uhakika, huku akielekeza bohari ya dawa nchini (MSD) kuhakikisha chanjo zote zimefika katika mikoa iliyosalia ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.
"Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wote nchini hakikisheni chanjo hizo mnazipeleka kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya na muwajulishe wananchi kwamba chanjo zipo na zinapatikana bila malipo yoyote, wazazi na walezi pelekeni watoto wenu kupata chanjo katika mikoa yenu" alisisitiza Dkt. Subi.
Chanzo: wizara_afyatz (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.