AFYA ya Halmashauri inategemea ushiriki wa watendaji wa kata katika kukusanya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mweka Hazina wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alfred Mlowe alipokuwa akiongea na watendaji wa Kata katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo.
Mlowe amesema “afya ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatutegemea sote, na inaanzia katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Yapo makusanyo yanayokusanywa na nyie watendaji wa kata na mengine yanasimamiwa na nyie”. Amesema kuwa baadhi ya watendaji Kata wanafanya kazi nzuri, lakini wengine hawakusanyi, hawafuatilii wala kuuliza mapato.
“Hatuwezi kutekeleza shughuli za maendeleo katika halmashauri kama hatukusanyi mapato. Hebu tuamke hii ‘council’ ni yetu sote, siyo ya Kunambi, Mlowe au Ngowi” amesema kwa ukali Mweka Hazina huyo.
Akiongelea usimamiaji wa mapato ya madini ujenzi, amewataka watendaji hao kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato katika madini hayo. “Kwenye madini ujenzi kuna fedha nyingi ila hazikusanywi, yawezekana wengine mnashirikiana kuhujumu mapato ya Halmashauri. Au mnataka mimi niende Mkonze kukusanya, je, Hombolo itakuwaje? Tumeanza mwaka wa fedha, tusaidiane kukusanya mapato ya serikali” ameongeza Mlowe kwa hisia kali.
Ametumia kikao hicho kuwakumbusha watendaji hao kuwa fedha zinazokusanywa na kata kutoka madini ujenzi asilimia 20 zinarudishwa kwenye Kata. Aidha, aliwataka watendaji kuhakikisha wanawalipa watu wanaokusanya fedha za madini ujenzi kwa wakati ili kufunga mianya ya upotevu wa fedha za Halmashauri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.