HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupitia Idara ya Elimu Msingi na Sekondari imeainisha mafanikio iliyoyapata katika sekta hiyo ndani ya kipindi kifupi na kutolewa kwa taarifa katika kikao cha Wadau wa elimu kilichofanyika leo Jijini Dodoma.
Akiainisha mafanikio hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji hilo, Afisa Elimu Sekondari Mwl. Upendo Rweyemamu amesema kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuendelea kuimarika kwa ubora wa huduma za kiutumishi kwa walimu na wadau wengine wanaotegemea idara ya Elimu Msingi na Sekondari, kuimarika kwa michakato ya ufundishaji na ujifunzaji kwenye shule za Msingi na Sekondari
Mwl. Rweyemamu amesema pia Halmashauri imeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na upatikanaji wa vifaa muhimu shuleni, huku ikiongeza uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika usimamizi na utoaji wa elimu bora.
“Halmashauri yetu haijaishia hapo imeendelea kutoa fedha za ulinzi, Maji na Umeme kwa shule zote za msingi na sekondari za serikali kwa fedha za mapato ya ndani yaani (Own Source)” Alisema Mwl. Rweyemamu.
Hata hivyo utoro, ukosefu wa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi, mimba kwa wanafunzi wa kike, ushiriki mdogo wa jamii katika mambo yanayohusu maendeleo ya shule na elimu ya watoto wao zimetajwa kama changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ndani ya Halmashauri hiyo.
Aidha Mwl. Rweyemamu ameongeza kuwa Halmashauri imeendelea kutenga fedha katika bajeti ya Halmashauri ya kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili kuimarisha na kuongeza idadi ya miundombinu na samani katika shule za Msingi na Sekondari.
“Licha ya changamoto tunazokutana nazo Halmashauri inaendelea kujenga vyumba vya madarasa 42, majengo ya utawala 6, utengenezaji wa meza na viti 5,000 na matundu ya vyoo 30 kwa Shule za Sekondari, huku kwa Shule za Msingi tunaendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa 22, utengenezaji wa meza na viti 2,352 na matundu ya vyoo 19”. Aliongeza Mwl. Rweyemamu.
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu akitoa maelezo ya mafanikio yaliyopatikana katika eneo la elimu Jijini Dodoma.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Mhe. Profesa Davis Mwamfupe (wa kwanza kulia) akiwa na wadau wengine wa elimu wakimsikiliza Mwalimu Upendo Rweyemamu akiwasilisha mada kuhusu hali ya elimu Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.