SERIKALI imebatilisha uamuzi wa kuwaondoa wanafunzi 48 wa shule za vipaji maalumu ambao walipata daraja la tatu katika mtihani wa ndani wa muhula wa pili wa kidato cha sita kwenda shule za bweni za kawaida baada ya kupoteza nafasi ya kuendelea na masomo kwenye shule hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa kwenye ziara kwenye shule ya Sekondari ya Kilakala ya wasichana wenye vipaji maalumu iliyopo mkoani Morogoro.
“Leo (Julai 19, 2019) nitoe tangazo la wazi kwa wanafunzi wote 48, kuwa Serikali imefanya tathmini na imeona wanafunzi wote hao waendelee na masomo yao kwenye shule hizo kwa mpango maalumu… haya ndiyo matunda ya Serikali inayowajali watu wote,” alisema Jafo.
Alisema TAMISEMI kupitia wataalamu wake walitoa barua kwenda kwa Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara ikiagiza juu ya uhamisho wa wanafunzi waliopata daraja la tatu hadi sifuri .
“Siku za hivi karibuni wataalamu wangu walitoa maelekezo kwenye shule za vipaji maalumu kwa waliopata daraja la tatu hadi ziro wanatakiwa wahamishwe kwenda shule za serikali za bweni za kawaida na kubakia waliopata daraja la kwanza na la pili,” alisema Waziri Jafo.
Alisema serikali imetafakari na imeona wanafunzi hao 48 waliopaswa kuondolewa waendelee kubaki kwenye shule hizo.
Hata hivyo alisema wanafunzi hao wametakiwa waongeze juhudi kubwa za kusoma na wakuu wa shule hizo pamoja walimu wao kuandaa mpango mkakati wa kuwawezesha kufanya vyema katika masomo yao.
Waziri Jafo alisema hayo ni maelekezo maalumu ya serikali na kwamba wanafunzi hao na wengine hawatakiwi kubweteka ila wanapaswa kujitambua kuwa kuchaguliwa kwenye shule za vipaji maalumu haikuwa ni kwa bahati mbaya isipokuwa ufauli wao ni wa kiwango cha juu na unapaswa kuendelezwa wanapokuwa kwenye shule hizo.
“Wanafunzi hawa wajiwekeee utaratibu wa kusoma kwa juhudi kubwa na walimu wa masomo yao waandae vipindi vitakavyowawezesha kufanya vyema sawa na wengine kupata alama za juu,” alisisitiza Mhe. Jafo.
Alisema lengo la serikali ni kuona matokeo ya mtihani mwaka 2020 shule zake zisizopungua sita zinaingia kumi bora na hilo litawezekana iwapo wanafunzi watazingatia masomo pamoja na wakuu wa shule kuweka programu maalumu zitakazosimamiwa na walimu ili kuwezesha ufaulu wa daraja la kwanza.
Jafo alisema shule za sekondari za kata hasa zenye kidato cha sita zina kuja kwa kasi kubwa na kati ya Shule 100 bora, shule 52 kati ya 64 za serikiali ni za Kata jambo ambalo linazitishia Shule 12 za vipaji maalumu.
Chanzo: HabariLeo Online
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.