CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) kimepunguza riba ya mikopo kutoka asilimia 15 hadi 13 kwa mwaka sawa na wastani wa asilimia 1.5 kutoka asilimia 2 kwa mwezi ili kuwawezesha wanachama wake kupata mikopo kwa gharama nafuu.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Hazina Saccos Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, ambaye hotuba yake ilisomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Gisela Mugumira aliyemwakilisha, alisema kuwa hatua hiyo italeta manufaa kwa wanachama wake.
“Nimefurahishwa na jambo hili la kushusha riba kwani ni mpango mkubwa wa Serikali kuona riba zinazotozwa na taasisi za fedha zinashuka zaidi ili kuinua maisha ya Watanzania, hivyo nawaelekeza muendelee kuona namna mnavyoweza kupunguza zaidi riba”, alisema Bi. Gisela.
Aidha, aliwataka viongozi na Bodi mpya itakayochaguliwa hapo kesho kuona ni namna gani itawawezesha wafanyakazi wote kufahamu na kujiunga na Hazina SACCOS, huku wakiongeza ubunifu wa bidhaa na huduma zinazolenga kutatua changamoto za wanachama na Watanzania kwa gharama nafuu.
Akizungumza kuhusu mpango wa Hazina SACCOS kuanza kuwalipia mikopo wanachama wanaodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Bi. Gisela, alipongeza hatua hiyo akieleza kuwa itasaidia wanafunzi wengi kupata mikopo kwani itaboresha ukwasi wa Bodi hiyo.
“Ubunifu huu ni vema ukatambuliwa, maana naona umelenga zaidi kuwasaidia wanachama wenu kulipa mikopo hiyo kwa mkupuo na wakati huo huo kutunisha mfuko wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.”Alieleza Bi Gisela.
Bi. Gisela, aliwaasa wajumbe wa mkutano kuwajibika na kuona kwamba Hazina SACCOS inasonga mbele na kukidhi mahitaji ya wanachama wake, huku ikiwa ya mfano kitaifa kwa sababu ndiyo SACCOS pekee nchini inayohudumia watumishi wote wa umma.
Aidha, alitoa rai kwa viongozi na wanachama kuongeza michango yao kila mwezi ili kuimarisha mfuko na kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi wa Hazina SACCOS anayemaliza muda wake Bw. Aliko Mwaiteleke alisema kuwa chama kimeendelea kutoa mikopo kwa wanachama wake ambapo mpaka kufikia tarehe 30 Septemba, 2020, jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 4.33 imetolewa kwa Wanachama 951 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali.
“Mikopo iliyotolewa mwaka huu ni sawa na ongezeko la asilimia 43 ambapo pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ukopaji tumelipa maombi ya mikopo yote kwa wakati kwa kuzingatia taratibu za Chama,” Alisema Bwana Mwaiteleke.
Bwana Mwaiteleke, alisisitiza umuhimu wa wanachama kurejesha mikopo kwa wakati kwani ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kupungua zaidi kwa riba ya mikopo kama wengi wanavyotamani.
“Bodi inatarajia kufanya mapitio ya riba na gharama za maombi ya mkopo ili iwe asilimia 13 kwa mwaka, mikopo ya dharura na 'standing order' iwe kati ya asilimia 0.5 na 1.5 kwa mwezi”, Alisema Bw. Mwaiteleke.
Aliongeza kuwa kwa kipindi cha miezi tisa chama kimekusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni 5 ikilinganishwa na kiasi cha Sh. bilioni 3.8 kilichokusanywa kwa kipindi kama hicho mwaka 2019.
Kwa upande wa uwekezaji Bw. Mwaiteleke alieleza kuwa uwekezaji kwenye mradi wa eneo la Njedengwa unaohusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kibiashara yakiwemo maduka makubwa, zoezi la kutafuta wawekezaji bado linaendelea na kamati ya uratibu wa mradi huo inaendelea na kazi hiyo.
Vile vile, katika kuboresha huduma za Chama, Chama kinaendelea zoezi la kujenga Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA utakao julikana kama Hazina SACCOS App, utakaowawezesha wanachama kupata taarifa zao kwa njia ya mtandao.
Hazina SACCOS ina wanachama takribani 5,000 ambao ni watumishi wa umma. Chama hicho kiko katika mkutano wa saba wa mwaka ambao unakutanisha wajumbe wa Mkutano Mkuu ili kupitia taarifa ya utendaji na maendeleo ya chama kwa kipindi cha miezi tisa kwa Mwaka 2020.
Meneja wa Hazina Saccos, Bw. Festo Mwaipaja, wakati wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina Saccos) katika Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi wa Mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali watu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Gisela Mugumira (walioketi-Katikati), akiwa pamoja na wajumbe wa Bodi ya Hazina SACCOS pamoja na Sekretarieti ya Chama hicho, wakati wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama hicho unaofanyika Ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es Salaam.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.