Na. Shaban Ally, Dodoma
Mwenyekiti Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Ngeze ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa soko la wazi la Machinga kwa lengo la kuwatengenezea mazingira rafiki ya biashara.
Pongezi hizo alizitoa alipoongoza timu ya ALAT taifa walipofanya ziara ya kutembelea mradi huo uliopo eneo la Bahi road jijini Dodoma.
“Kwa niaba ya ALAT, nikushukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na viongozi wengine wa jiji kwa kuupiga mwingi. Lakini nikuombe mheshimiwa mkuu wa mkoa kuzingatia suala la usalama katika eneo hili la mradi ili kuepusha usumbufu kwa wafanyabiashara”, alisema Ngeze.
Ngeze aliushauri uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuzingatia maendeleo ya kiuchumi kwa wafanyabiashara hao kwa kuwapa elimu ya biashara ili kuweza kuwakomboa kiuchumi. “Nikuombe mheshimiwa mkuu wa mkoa uweke utaratibu wa mafunzo ya biashara kwa wafanyabiashara hao kwa lengo la kuwaendeleza” aliongeza Ngeze.
Ngeze alihitimisha kwa kuwaomba viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hususani wajumbe wa ALAT, kwenda kujifunza miradi ya maendeleo katika Halmashauri yake ya Kagera ili kupanua mawazo ya kimaendeleo kwa viongozi hao.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia halmashauri yake kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kuendeleza ujenzi wa mradi huo.
Naibu Meya aliwaomba viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na ALAT kudumisha umoja na ushirikiano baina yao ili kuchochea maendeleo zaidi. “Niwaombe ndugu viongozi wenzangu kwa pamoja tudumishe umoja wetu na ushirikiano ili asije akatokea mtu yeyote wa kuvunja umoja wetu”, alisema Chibago.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka akimuonyesha Mwenyekiti Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Murshid Ngeze moja ya aina ya vizimba vitakavyotumika katika Soko la wazi la wamachinga jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.