Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma imefurahia juhudi za uongozi wa Kata ya Hombolo Makulu kuhamasisha wananchi kushiriki katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu iliyofikia asilimia 90.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Dkt. Damas Mkassa (pichani juu) alipoongoza Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu iliyopo jijini Dodoma.
Dkt. Mkassa alisema “niwapongeze viongozi wa Kata ya Hombolo Makulu akiwemo Mheshimiwa Diwani wetu na Afisa Mtendaji wa Kata. Lakini pia wananchi na viongozi wa eneo hili kwa kutoa ushirikiano sababu nimesikia hapa kuna nguvu ya wananchi. Bila wananchi kuhimizwa kutoa nguvu zao hapa tusingefikia hii hatua ambayo tumefikia. Kwa hali halisi, mradi huu nafikiri umevuka asilimia 90, kwa maana hiyo tunatarajia mwakani mapema sana wanafunzi watakaofaulu wataweza kutumia shule hii”.
Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa fedha anazotoa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. “Mkoa wa Dodoma ni mkoa wa mfano, katuletea miradi mingi na mingine tutaiona baadae. Lakini huu ni mfano mzuri wa kuigwa taarifa inaonesha wanafunzi walikuwa wanatembea zaidi ya kilometa tisa kufuata elimu. Kwa maana hiyo, tutakuwa tumewakomboa watoto wetu na hasa wa kike ambao wanakuwa kwenye maeneo hatarishi kwa kwenda kutafuta elimu mbali. Lakini pongezi za pili nizitoe kwa uongozi wa Wilaya ya Dodoma, Jiji la Dodoma Mkurugenzi wetu, Joseph Mafuru na timu yake ya wataalam kwa kusimamia vizuri ujenzi wa mradi huu” alisema Dkt. Mkassa.
Aidha, alishauri TARURA kuchonga barabara inayoelekea shuleni hapo ili irahisishe kusafirisha vifaa na wakaguzi kwenda kukagua shule hiyo.
Vilevile, alishauri kuchimbwa kisima katika shule hiyo ili kuwa na maji ya uhakika na kuepuka kunyang’anyana maji na wananchi.
“Suala la tatu ni umeme, nimeambiwa umeme hapa haujafika. TANESCO ni yetu na ipo mkoani kwetu, tutawaomba wakamilishe miundombinu ya umeme. Umeme utaimarisha usalama hapa, na maabara tatu tulizoziona hapa zitategemea umeme kufanya kazi, masomo ya kompyuta pia yatategemea umeme kufanya kazi. Kwa ujumla sisi Kamati ya Siasa ya Mkoa, mimi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa tumeuona mradi na tumeupokea vizuri. Mradi ni mzuri unatia moyo na tunatoa pongezi kwa Mwenyekiti wetu wa CCM na Rais wa Jamhuri wa Jamhuri kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa Dodoma” alisema Dkt. Mkassa.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu, mkuu wa shule hiyo, Joseph Kavarambi alisema kuwa ujenzi ulianza tarehe 25 Januari, 2022 kwa ufadhili wa mradi wa kuboresha elimu ya sekondari “SEQUIP” kwa gharama ya shilingi 600,000,000 mpaka utakapokamilika. Alisema kuwa katika awamu ya kwanza shilingi 470,000,000 zilitolewa.
Kavarambi alisema kuwa ujenzi huo unatumia utaratibu wa force account, awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, jengo la utawala, maabara tatu za sayansi, jengo la ‘ICT’, maktaba na matundu 20 ya vyoo.
Alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo utawasaidia wanafunzi kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia. Mradi umetoa ajira kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani kwa kushiriki katika kazi za ujenzi na uuzaji vyakula.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea mradi huo. “Mheshimiwa mwenyekiti mimi nakushukuru sana kufika eneo hili la Hombolo Makulu na kufanya ukaguzi, lakini pia kutoa tathmini ya ukaguzi wako kwa namna ya kisomi sana, katika masuala ya msingi sana ambayo umeyasema. Kwa niaba ya wenzangu wote kwenye msafara huu tunakushukuru sana kwa maoni na maelekezo ambayo umeyatoa na tunakupongeza kwa kufanya kazi kwa weledi.
“Lakini ni sahihi kabisa na sisi tunaungana na viongozi wa chama mkoa kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kututengea fedha na kutupatia shilingi 600,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari ya Hombolo Makulu. Taarifa unayo, lakini tukili tulipokea shilingi 470,000,000 za awali na zikafanya kazi kwa kiwango hiki unachokiona. Ujenzi wa madarasa nane ambayo yanakiwango kizuri sana, ujenzi wa maktaba, shule hii itakuwa na maktaba ya kisasa sana. Ujenzi wa chumba cha kompyuta na ujenzi wa maabara tatu pamoja na maeneo ya maliwato kwa wanafunzi wetu na wenye mahitaji maalum pamoja na chumba cha kubadilishia” alisema Shekimweri.
Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa maono mapana ya Rais. “Zaidi ya kutupatia shilingi bilioni 2.86 kwa Jiji la Dodoma ya kujenga madarasa ya UVIKO-19, bado katupatia shilingi 600,000,000 ya kujenga hii shule ya Hombolo Makulu. Mheshimiwa Rais katika wilaya yetu hii, Jiji kaliweka kwenye moyo wake na sisi tunaemsaidia majukumu katika maeneo haya tumhakikishie tutaendelea kusimamia fedha hizi vizuri na muda wote tupo ‘site’ kusimamia fedha hizi” alisisitiza Shekimweri.
Akiongelea changamoto za maji, barabara na umeme, alisema kuwa wilaya yake inazifahamu. “Nikuhakikishie tunazifahamu na wadau wote wapo hata. Nguzo zimeshaanza kuja hapa. Ni jambo la muda, tuna muda mrefu hadi kufikia Desemba, maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hapa shuleni. Tumeshatoa maelekezo ya kuanza taratibu za usajili wa shule hii” alisema Shekimweri.
Nae mzazi Agatha Kihori alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo ni mkombozi kwa wanafunzi wa Kata ya Hombolo Makulu. “Wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu sana kwenda shule. Kuna wakati mzazi unafikiria mtoto atarudi kweli salama. Tunaishukuru sana serikali kwa ujenzi wa shule hii” alisema Kihori.
Ukamilishaji wa shule ya sekondari Hombolo Makulu utaifanya Kata ya Hombolo Makulu kuwa na shule yake ya kwanza ya sekondari.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma walipotembelea na kukagua ujenzi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu iliyopo jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.