MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mikakati ya upandaji miti baada ya kugawanya Wakuu wa Idara wa Halmashauri hiyo katika Mitaa mbalimbali kusimamia zoezi la upandaji miti jambo ambalo litaongeza kasi ya zoezi hilo Jijini hapa.
Dkt. Mahenge ameyasema hayo leo alipoongoza zoezi la upandaji miti katika Kata ya Mkonze Mtaa wa Miganga ambapo zaidi ya miti 2000 imepandwa katika eneo hilo.
Aidha, Dkt Binilith Mahenge amewataka viongozi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kujenga utaratibu wa kutembelea na kufuatilia maeneo yote yanayopandwa miti kuona maendeleo ya miti hiyo kama inahudumiwa ili kuona matokeo mazuri ya zoezi hilo.
Dkt Mahenge amesema zoezi hilo ambalo mwitikio wake umekuwa mzuri lakini kama ufuatiliaji hautafanywa hakutakuwa na matokeo yaliyotarajiwa.
“Zoezi hili ni zuri sana lakini kama hatufanyi ufuatiliaji zoezi hili halina maana, hakikisheni mnafuatilia maeneo yote yaliyopandwa miti ili kuona namna inavyoendelea” amesema Dkt Mahenge.
Vile vile, amewapongeza Wananchi wa Mtaa wa Miganga kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri, Meneja TARURA na TANESCO kuhakikisha wanatoa kipaumbele kupeleka huduma zote muhimu katika eneo hilo huku akisema kuwa hayo ndio matunda na faida za kuwa wazalendo na kujitokeza kufanya mambo ya kijamii.
“Nataka mtaa huu upewe kipaumbele na ninaanza na eneo hili tulipo hii ilikua barabara kubwa ya Mkoa lakini imetelekezwa hivi, hivyo natoa siku tano kwa TARURA kuhakikisha barabara hii inapitika, lakini pia huduma ya umeme na upimwaji wa viwanja uzingatie sana mtaa huu kwa sababu wamejitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali za kukijanisha Dodoma.” Alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Joseph Mafuru amesema kuwa leo wameonesha aina nyingine ya upandaji wa miti kwa kupanda pembezoni mwa barabara tofauti na ilivyozoeleka katika Jumamosi zilizopita lengo ni kuufanya mji uwe katika mandhari nzuri na kuweka vivuli katika barabara za Jiji hilo.
Mafuru ameongeza kuwa jumamosi ijayo ni ya usafi lakini hilo haliwazuii wao kuendelea kupanda miti kwani zoezi hilo pia ni miongoni mwa njia mojawapo ya kutunza mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinilith Mahenge akiongea na wananchi waliojitokeza kwenye zoezi la kupanda miti Mtaa wa Miganga Jijini Dodoma. Dkt. Mahenge aliongoza zoezi hilo ambao lilifanyika asubuhi ya leo.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akiongea kuhusu mikakati ambayo Halmashauri imejiwekea ili kuhakikisha zoezi la kukijanisha Dodoma linafanikiwa.
Mkuu wa Idara ya Usafi wa Mazingira na udhibiti wa taka ngumu wa Jiji Dickson Kimaro akifafanua jinsi Jiji lilivyojipanga pamoja na TFS kuhakikisha miche ya miti inapatikana kwa ajili ya kulifanikisha zoezi la kukijanisha Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.