HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa juhudi za kuinua kiwango cha taaluma kwa elimu ya msingi kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu na uwekezaji katika rasilimali watu.
Pongezi hizo zilitolewa na Meneja mradi wa Mkoa wa Dodoma kutoka mradi wa Tuimarishe Afya -Health Promotion System Strengthening (HPSS), Kenneth Gondwe, katika hotuba yake iliyosomwa na Dennis Harrison katika mahafali ya kuhitimu elimu ya msingi kwa shule ya msingi Chihoni iliyopo kata ya Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma jana.
Gondwe alisema kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi. “Nimetaarifiwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejenga madarasa mawili shuleni hapa. Halmashauri pia imetoa matofali 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa matano, na matofali 3,000 yamekwisha fika shuleni hapa. Juhudi hizi zinalenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Shukrani kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Baraza la Madiwani kwa mipango mizuri ya kuboresha mazingira ya elimu katika shule za Jiji” alisema Gondwe. Alieleza matarajio yake kuwa mamlaka husika zitahakikisha matofali hayo yanafika mapema ili ujenzi na ukamilishaji wa majengo ya madarasa hayo ukamilike na wanafunzi waanze kuyatumia na kuondoa msongamano wa wanafunzi katika madarasa.
Meneja huyo aliwapongeza wanafunzi wote ambao wanatarajiwa kuanza mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi tarehe 11-12 Septemba, 2019 na kusema wamechagua fungu lililo jema. “Napenda kuwapongeza wanafunzi wote ambao leo ni mahafali yenu. Najua haikuwa rahisi sana kufikia hatua hii. Mmefanya kazi kubwa na kujituma. Hongera kwa walimu kwa kazi nzuri ya kuwaandaa na kuwalea wanafunzi hawa. Maandalizi mliyowapa ni mazuri” alisema Gondwe.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Chihoni, Eliah Malugu aliwataka wanafunzi hao kuwa watulivu watakapokuwa wakifanya mitihani yao. “Huu ni mwanzo, tunategemea wengi mtafaulu na kwenda sekondari ya Nala” alisema Malugu. Aidha, aliwataka wazazi kuacha kauli za kuwakatisha tamaa wanafunzi wanaosoma shule za kata.
Katika risala kwa mgeni rasmi ya wanafunzi wahitimu iliyosomwa na Sophia Julius, alisema kuwa wanafunzi hao wamepata elimu bora yenye kutoa muelekeo bora wa maisha. “Kila muhitimu katika nyanja zote yaani nadharia na vitendo, hii inatupa ujasiri wa kuwa na uchaguzi bora wa taaluma tutakazozitumikia baadae mfano ualimu, udaktari, uuguzi, uhandisi n.k” alisema Julius.
Shule ya msingi Chihoni ilianza mwaka 1953, hivi sasa inawanafunzi 924, wakati wanafunzi wanaohitimu darasa la saba ni 83.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.