Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma imeipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekeleza takwa la kisheria la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kutoka mapato ya ndani kwenda kwa makundi maalum.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma, Sophia Kibaba wakati wa majumuisho ya ziara ya siku tatu ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma yaliyofanyika katika ofisi ya CCM Wilaya.
Kibaba alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inafanya vizuri katika utekelezaji wa utoaji mikopo ya asilimia 10 kutoka katika mapato ya ndani. “Pongezi kwa Jiji la Dodoma kwa kazi kubwa ya mikopo ya asilimia 10 ya makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Sehemu nyingi mikopo inayokopeshwa ni kidogo na haizidi shilingi milioni tano” alisema Kibaba.
Alisema kuwa vikundi vinapokopeshwa fedha kidogo vinashindwa kujiendesha. “Mkopo ukitolewa mkubwa unakuwa na tija zaidi kwa uendeshaji vikundi. Niwapongeze pia kwa utaratibu wa kuvifuatilia vikundi vilivyokopeshwa ili vistawi zaidi na kufanya marejesho kwa muda uliopangwa” alisema Kibaba.
Akiongelea ushirikiano baina ya CCM na Serikali, alisema kuwa ushirikiano huo ni mzuri. “Serikali msisubiri ziara za chama ili ziibue na kutatua changamoto. Kama kuna jambo linahitaji utayari na ushiriki wa CCM, basi tuwasiliane mapema ili tutoe ushauri au maelekezo ya utekelezaji. Ni vizuri zaidi chama kuwa sehemu ya utekelezaji wa mipango ya serikali. Milango ya CCM Wilaya ipo wazi ili nyumba tunayojenga iendelee kukomaa” alisema Kibaba kwa kumaanisha dhamira thabiti.
Kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya CCM wilaya, alisema kuwa serikali inatakiwa kuyatekeleza na kutoa mrejesho wa hali ya utekelezaji. “Tunapotembelea miradi ya maendeleo na kutoa maelekezo, tunataka utekelezaji wake uwe wa haraka. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ipo haraka sana kujibu utekelezaji wa maelekezo ya CCM. Tunapenda kuona matokeo chanya ya utekelezaji wa maelekezo ya CCM kwa serikali yake” alisema Kibaba kwa msisitizo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.