Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa uongozi bora na kutoa fedha shilingi 6,109,748,702.50 za tozo ya Mafuta kujenga barabara ya Nzuguni - Mahomanyika kilometa 5.0 kwa kiwango cha lami.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Damas Mkassa alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nzuguni Mahomanyika inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Dkt. Mkassa alisema “nitangulize shukrani na pongezi kwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora na kazi nzuri. Fedha hizi nasikia zimetokana na tozo ya mafuta na kuna watu walikuwa wanapiga kelele juu ya tozo ila tunaona matokeo makubwa ya hizo tozo. Na siku zote mkuu wa nchi anapotoa maelekezo anakuwa ameona mbali. Tunaweza tusione matokeo mwanzo ila tunaweza kuona sasa hizi kilometa za barabara zinakwenda kujengwa hapa. Barabara hii ina umuhimu mkubwa sababu inatuunganisha na vitu vikubwa. Inatuunganisha na barabara kuu ya Dar es Salaam, inatuunganisha na Soko kuu la Job Ndugai, kutuo kikuu cha mabasi Dodoma hadi ‘ring road’ na hadi nyumba 350, ni muhimu sana kwa barabara hizi zinapokuwa katika jiji”.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nzuguni Mahomanyika (kilometa 5.0) kwa kiwango cha lami, Mhandisi wa TARURA, Revocatus Nsubile alisema kuwa mradi huo upo chini ya Mkandarasi Nyanza Road Works co Ltd.
Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi 6,109,748,702.50. “Mkataba una miezi 12 na ulianza tarehe 5.4.2022 na unatarajiwa kukamilika tarehe 5.4.2023. Mradi una asilimia 28 zaidi ya asilimia 23 kiwango mradi uliotakiwa kuwa sasa. Hadi sasa hakuna mabadiliko ya gharama ya mradi na hatutarajii kuyapata” alisema Mhandisi Nsubile.
Akitoa ufafanuzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema kuwa barabara hiyo ni ya kimkakati. “Mradi huu ulikuwa chini ya TARURA kwa ujenzi wa kilometa 1.55 lakini kwenye ziara ya Waziri wa Nchi- TAMISEMI, tuliweza kumpatia taarifa na nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye aliwasilisha ombi kwa serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii kimkakati. Barabara hii inaunganisha mashamba ya mjini ‘urban farms’ ya Hombolo pamoja na Vikonje lakini inaunganisha makazi mapya yanayojengwa na TBA nyumba 350, lakini pia inatuunganisha na uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Msalato ambao upo kwenye ujenzi. Babaraba hii inaunganisha na barabara ya Pete ya mzunguko, ni barabara inayotuunganisha na Soko Kuu la Job Ndugai, Kituo Kikuu cha Mabasi ya mikoani, lakini pia uwanja wa maonesho wa Nanenane lakini pia uwanja wa mpira utakaojengwa Nzuguni” alisema Shekimweri.
Mkuu wa wilaya aliitaja barabara hiyo kuwa ya kipekee. “Baada ya hoja hiyo, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa TAMISEMI na waziri aliyatamka hapa kwamba tutaogezewe kilometa tano na hivyo, kujenga kwa kiwango cha lami nusu ya barabara hii kilometa 13. Ni matarajio yetu barabara hii ikikamilika kilometa 6.5 kwa bajeti inayokuja itaendelea kuwa kipaombele ili iweze kufikia matarajio ambayo kila mtu anayo” alisema Shekimweri.
Aidha, alimpongeza Diwani wa Kata ya Nzuguni kwa kazi nzuri na kutoa ushirikiano mkubwa kwenye kuwaelimisha wananchi kulinda mradi huo.
Jeremiah Chongo ambae ni mkazi wa Mahomanyika alisema kuwa barabara hicho itachangia kukuza uchumi wa maeneo mbalimbali ya jiji hilo. Alisema kuwa ujenzi wa barabara kama ulivyo ujenzi wa miundombinu mingine ni kichocheo cha maendeleo ya maeneo mbalimbali kwa sababu inafungua fursa za kibiashara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.