Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuimarisha miundombinu na maslahi ya watumishi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma jambo lililoamsha ari ya kazi kwa watumishi hao.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma katika tukio hilo, Joseph Mafuru alipotoa neno kwa niaba ya Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mkoa wa Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF leo katika hafla ya kumshukuru na kumpongeza Rais kwa kuboresha maslahi ya watumishi.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anaimarisha miundombinu kwa kasi kubwa. “Mimi kama mkuu wa taasisi wa Jiji la Dodoma ninaona sura na kazi ya utendaji ilivyobadilika mapema baada ya kusikia matangazo ya nyongeza ya mshahara. Watumishi unawaona wanafanya kazi kwa kasi. Ukienda kwenye kata unawakuta, ukienda kwenye mitaa unawakuta wanasimamia miradi ya maendeleo kwa kasi kubwa. Hii inatasfiri kubwa sana kwamba morali imerudi juu. Maana yake tutegemee matokeo kubwa kwenye huduma za wananchi na huduma za jamii kwa ujumla” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Alisema kuwa kuanzia mwezi Julai mambo mengi yanakwenda kubadilika baada ya mishahara kubadilika. “Tuna madeni mawili, moja kasi ya utoaji wa huduma za uhakika lazima tuoneshe nini kimebadilika kwetu, isije fika mwezi Agosti au Septemba, wananchi wanaona huduma ni ileile kama ambavyo ilikuwa miaka miwili ya nyuma” alisema Mafuru.
Mwenyekiti huyo wa Wakurugenzi wa Mkoa wa Dodoma alisema kuwa Rais ameendelea kuboresha miundombinu kwa ujenzi wa barabara ya mzunguko “ring road” inayozunguka Jiji la Dodoma. “Tafsiri yake ni kwenda kufungua uchumi pembezoni mwa Jiji la Dodoma. Maana yake nyongeza ya mishahara ipo, kuna watu wana “arreas” mpaka milioni 40 na milioni 20 katika akaunti zao. Maana yake twende tukafanye uwekezaji. Twende tukajenge viwanda, hoteli na vituo vya Mafuta kwa ajili ya faida yetu na pili kwa ajili ya kuzalisha ajira” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga alisema kuwa hafla hiyo ililenga kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nyongeza ya mishahara na posho za wafanyakazi. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ulielekeza kuwa leo tukutane watumishi wote ambao tumepata bahati ya kupata ajira serikalini, tunakutana hapa kwa jukumu kuu moja, sisi sote ni watanzania tumepata ajira ya kuwatumikia watanzania wenzetu. Lakini imepita miaka mingi tokea watumishi hawa waweze kupata nyongeza katika mishahara yao. Lakini kama haitoshi, posho za kufanya kazi mbalimbali, posho za safari zimekuwa katika kiwango hicho ambacho tunacho kwa muda mrefu sana kwa kupitia mawazo ya Mkuu wa Mkoa akasema ni busara tukutanike hapa kwa ajili ya kumpoongeza na kumshukuru Rais Samia kwa hiki alichokifanya kwa wananchi wote” alisema Dkt. Mganga.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.