MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ameridhishwa na mwanzo wa utekelezaji wa agizo lake kwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma la kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Dkt. Mahenge alionesha kuridhishwa alipokuwa akitoa salamu za shukrani baada ya kukamilika kwa zoezi la upandaji miti lililochukua masaa matatu katika eneo la Iseni Park jijini hapa.
“Napenda kuwapongeza na kuwashukuru sana kwa mwitikio wenu katika zoezi hili la upandaji miti. Wingi huu umelifanya zoezi la upandaji miti kuwa jepesi na kitendo cha furaha kwetu sote. Leo tumepanda miti zaidi ya 3,700 kutokana na umoja tulionao. Tukiwa na nguvu hii kwa kata zote Dodoma ya kijani tunaifikia mapema zaidi. Hivyo, nimeona ni jambo la uungwana watu wakifanya kazi nzuri kupewa shukrani” alisema Dkt. Mahenge.
Aidha, alipongeza mkakati wa halmashauri hiyo wa kuzishirikisha ofisi za kata kwenye zoezi la upandaji miti katika maeneo yao. “Ni vizuri halmashauri ikasimamia utekelezaji na tujitahidi kila mtu amuombe Mungu kwamba apate nguvu ya kuwajibika kuitunza sayari yetu ili tupate vile ambavyo tunavihitaji katika sayari hii. Miti hii tunayopanda inaenda kuvuna hewa ukaa. Dodoma ya kijani itawezekana kama nguvu yetu hii iliyojitokeza leo kuja kupanda miti itaendelea kujitokeza na kushiriki katika mazoezi ya kupanda miti. Ndiyo maana tukaona sisi kama viongozi lazima tuoneshe njia kwa kujitokeza mara kwa mara katika mazoezi ya upandaji miti ili kutoa hamasa kwa jamii” alisema Dkt. Mahenge.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa kazi iliyoanza wiki iliyopita ya kupanda miti. “Hili eneo Iseni park zamani ndilo lilipangwa kuwa makao makuu, yaani mji wa serikali mtumba ‘National Capital Center’ kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa mwaka 1976. Maamuzi ya sasa, eneo hili zijengwe ofisi za wizara na zitakazo baki zitapelekwa eneo la Kizota ambazo ni kubwa kama eneo hili” alisema Mafuru.
Wakati huohuo, Mkuu wa Idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu katika Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa zoezi la upandaji miti ni endelevu kwa lengo la kukijanisha Dodoma. “Eneo hili lina ekari 37, ni eneo la wazi. Leo kuna mashimo 3,700 na miti iliyokuja hapa ni 4,000. Tukumbuke kuwa katika mji mikubwa kuna misitu ya mjini kwa lengo la kuusaidia mji kupumua na kuondoa uharibifu wa mazingira kwa njia ya hewa” alisema Kimaro.
Joseph Fungo, ambae ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA na Uhusiano katika Jiji la Dodoma alisema kuwa zoezi hilo ni zuri kwa mustakabali wa Jiji hilo. “Kama unavyofahamu ni wajibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa huduma kwa wananchi na kupendezesha Jiji la Dodoma. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alitoa agizo kwa watumishi wote kushiriki katika zoezi la upandaji miti. Kitengo chetu kama sehemu ya halmashauri tulihakikisha watumishi wote na wananchi wanapata taarifa ya zoezi hili ili wafike eneo hili kwa ajili ya kupanda miti. Matangazo ya barabarani, tovuti, mbao za matangazo na mitandao ya kijamii ili kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa” alisema Fungo. Zoezi hilo siyo la watumishi wa jiji pekee, ni jukumu la jamii nzima, aliongeza.
Ikumbukwe kuwa tarehe 9 Januari, 2021 mkuu wa mkoa wa Dodoma alipokuwa akizindua zoezi la upandaji miti katika utekelezaji wa kampeni ya kijanisha Dodoma aliagiza kila mtumishi wa Jiji la Dodoma kupanda miti 10 kila wiki katika majira ya mvua.
Afisa Habari wa timu ya Dodoma Jiji FC, Moses mpunga akipanda mti eneo la Iseni Park Jijini Dodoma.
Mchumi Jiji la Dodoma, Shaban Juma akipanda mti eneo la Iseni Park Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.